NA RAJAB MKASABA, IKULU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amefutari na wananchi wa mkoa wa Kusini Pemba na kuwataka kuendelea kuiombea nchi amani.
Hafla hiyo ya futari iliyoandaliwa kwa wananchi wa mkoa huo, ilifanyika katika ukumbi wa kiwanja cha kufurahishia watoto Tibirinzi, kilichopo Chake Chake, ambapo ilihudhuriwa na baadhi ya viongozi wa serikali, dini, vyama vya siasa na makundi maalum ya wananchi wa mkoa huo.
Katika maelezo yake, Dk. Mwinyi aliwasisitiza wananchi wa Zanzibar kuendelea kuiombea nchi amani sambamba na mshikamano ili iweze kujiletea maendeleo zaidi.
Aliwapongeza wananchi wa mkoa huo kwa kukubali mualiko wake na kuhudhuria hafla hiyo ya futari aliyowaandalia wananchi wa mkoa huo ambayo aliwakilishwa na wenzao.
Aidha, Dk. Miwnyi alieleza kwamba ameona umuhimu wa kuandaa futari hiyo ili aweze kuungana na wananchi wa Mkoa huo katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Nao wananchi wa mkoa wa Kusini Pemba wakitoa shukurani kupitia Omar Khamis Othman, alieleza kufarajika na mwaliko huo waliopewa na Dk. Mwinyi kwa niaba ya wenzao wa Mkoa huo.
Wananchi hao waliipongeza hatua hiyo ya Dk. Mwinyi kwa lengo lake la kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar ambapo mkusanyiko huo unaonesha dhahiri nia yake hiyo njema.
Aidha, wananchi hao walitoa shukrani kwa Mama Mariam Mwinyi kwa kuungana na wananchi wa Mkoa huo katika futari hiyo maalum aliyoiandaa Dk. Mwinyi.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Matar Zahor Massoud kwa upande wake alieleza kwamba jambo alilolifanya Alhaj Dk. Mwinyi ni jambo kubwa na kumuombea dua kwa moyo wake huo wa kuwafutarisha wananchi wa mkoa huo.
Nae Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi kwa upande wake aliungana na viongozi wanawake wa kitaifa pamoja na wananchi wa Mkoa huo wa Kusini Pemba katika futari hiyo maalum aliyoianda Dk. Mwinyi hapo katika ukumbi wa Uwanja wa Kufurahishia watoto Tibirinzi, Pemba.
Wakati huo huo, Dk. Mwinyi aliungana na waumini wa dini ya kiislamu wa mkoa huo wa Kusini Pemba katika sala ya taraweh katika Masjid Al Rahmaan uliopo Gombani Chake Chake Pemba.
Dk. Mwinyi alimuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuipa Zanzibar amani, umoja na maendeleo huku akieleza furaha yake kwa kufika Pemba na kukutana na waumini na wananchi.