Aahidi kupandisha mishahara ngazi ya kati

KHAMISUU ABDALLAH NA LAYLAT KHALFAN

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema serikali ya Mapinduzi Zanzibar inathamini na kutambua mchango wa wafanyakazi katika kufanikisha harakati za maendeleo.

Kauli hiyo aliitoa katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani inayoadhimishwa kila ifikapo Mei Mosi ya kila mwaka katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul- wakil Kikwajuni.

Alisema mafanikio ya utendaji wa serikali kwa kiasi kikubwa yanategemea mchango wa wafanyakazi katika kutekeleza wajibu wao na kuwatumikia wananchi kwa misingi ya haki, usawa na uwajibikaji.

Aidha alisema wafanyakazi wa kada zote kupitia shirikisho la vyama huru vya wafanyakazi Zanzibar, ni wadau muhimu wa maendeleo ya nchi na ndio injini ya kufikia mafanikio yote yanayotarajiwa.

Dk. Mwinyi alibainisha kuwa katika hotuba aliyoitoa wakati akifungua Baraza la Wawakilishi Novemba 11 mwaka jana alieleza dhamira na mategemeo ya serikali ya awamu ya nane kwa wafanyakazi hasa kwa watumishi wa umma.

Aliwahakikishia kuwa dhamira njema ya serikali ni kuhakikisha haki na maslahi yote yanazingatiwa na kupatikana sambamba na kuimarishwa mazingira mazuri ya kazi.

Alibainisha kuwa kwa vile haki na wajibu ni watoto pacha, aliwahimiza wafanyakazi kutekeleza wajibu wao kwa bidii na nidhamu ili kufikia dhamira ya kukuza uchumi na kuimarisha huduma za jamii kwa lengo la kuleta maendeleo nchini.

Hata hivyo alisema serikali kupitia mikutano mbalimbali ikiwemo ya wadau na taarifa zinazotumwa kupitia mawasiliano ya sema na rais, wamebaini kero zinazolalamikiwa na wananchi wengi wakiwemo watumishi wa umma.

Akizungumzia suala la ugatuzi na bima ya afya alisema tayari serikali imelifanyia kazi huku akiahidi kuendelea kulifanyia kazi suala la bima ya afya.

Alisema, maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani yana umuhimu mahsusi katika kutathmini harakati za maendeleo ya nchi na siku ya kubainisha changamoto zinazowakabili wafanyakazi katika utekelezaji wa majukumu yao, namna ya kukabiliana nazo kwa lengo la kuongeza ufanisi.

Alisema, siku hiyo pia ni ya kukumbushana na kuhimizana wajibu wa wafanyakazi katika kutekeleza majukumu yao katika utumishi na kuchochea maendeleo ya nchi katika sekta mbalimbali.

Alibainisha kuwa katika kipindi kifupi cha uongozi wa serikali ya awamu ya nane imeanza vyema utekelezaji wa malengo yake kwa mujibu wa mipango mikuu ikiwemo ilani ya CCM 2020/2025, Mkuza 111 na Dira ya Zanzibar ya mwaka 2020/2050 na mambo mengine ya kisekta na kimataifa.

Alisema hali ya nidhamu na uwajibikaji wa watumishi serikali imeendelea kuimarika, nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kiasi kikubwa inazingatiwa kwa kuepuka kufanya matumizi kinyume na utaratibu, kuziba mianya ya mapato kwa kutumia mifumo ya kisasa.

Dk. Mwinyi aliutaka uongozi wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji kushirikiana na ZATUC katika kuendelea kusimamia haki za wafanyakazi kwani wapo waajiri wanaopuuza wajibu wao wa kutimiza haki za wafanyakazi wao.

Akizungumzia suala la mishahara alisema hali ya uchumi ikiimarika kidogo basi serikali itaendelea kuongeza mishahara kwa kada ya kati kwani wanastahili kufikishwa katika kupata maslahi mazuri.

Aliahidi kuwa taratibu na tathmini ya miundo ya utumishi serikalini zitaendelea kushughulikiwa ili kuhakikisha watumishi wote wanapata haki zao na kuwa na mazingira bora ya kufanyia kazi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Sambamba na hayo, aliahidi kuliangalia upya suala la pencheni kwa kina ili kuona lengo la serikali wananchi wananufaika hususani waliotumikia nchi kwa muda mrefu na kuona wanapata kiinua mgongo na sio kivunja mgongo.

Kwa upande wa wastaafu na wazee alisema serikali itaendeleza jitihada zilizoanzishwa kwa kuimarisha maslahi yao kwa kadri hali ya uchumi inavyozidi kuimarika huku kuhakikisha malipo ya viinua mgongo kwa wastaafu na pencheni jamii zinaendelea kutolewa kwa wakati bila ya usumbufu.

Akisoma risala ya wafanyakazi Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar, Mwatum Khamis Othman, alisema nchi imepiga hatua kubwa katika kupigania haki, maslahi na ushirikishwaji wa wafanyakazi toka Mapinduzi ya mwaka 1964 ukilinganisha na nchi nyengine duniani.

Alisema, pamoja na mafanikio hayo wafanyakazi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukimya wa serikali katika suala la uwezekano wa kupandisha kima cha chini cha mishahara na pencheni.

Changamoto nyengine alisema ni kukosekana kwa utaratibu mzuri wa upandishaji wa madaraja na nyongeza za mwaka pamoja na posho la mazingira magumu katika kada muhimu na taasisi zinazojitegemea.

Alisema matatizo yaliyojitokeza kutokana na marekebisho ya mishahara ya mashirika ya umma, mamlaka na taasisi zinazojitegemea mwaka 2019 ambapo baadhi ya mafao ya wafanyakazi yalifutwa kwa wafanyakazi wa chini na kuongezwa kwa wafanyakazi wa ngazi za juu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Waajiri Zanzibar (ZANEMA), Salah Saleh Salah, alisema umefika wakati wafanyakazi kujitathmini katika siku hiyo kwani bado kuna mambo kadhaa yamekuwa yakifanywa katika sehemu za kazi ikiwemo kutokamilisha masaa ya kazi dharura na visingizio visivyokwisha, kuingia kazini  na kutoka muda wanaotaka.