Asema kazi anayofanya ni kuziba mianya

Abainisha anapotumbua hamuonei mtu

NA KHAMISUU ABDALLAH

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema kwa kipindi cha miezi sita ya uongozi wake anashindwa kupata usingizi kutokana na mambo aliyoyakuta serikalini ikiwemo upotevu mkubwa wa mapato ya serikali.

Dk. Mwinyi ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliyasema hayo jana wakati akizungumza na viongozi wa halmashauri kuu za matawi, wadi jimbo na wilaya wa mkoa wa Kaskazini Unguja katika ukumbi wa ofisi ya chama hicho Mkoa wa Kaskazini Unguja Mahonda.

Alisema katika kipindi hicho amefanya kazi ya kuunganisha wazanzibari kudhibiti suala la mapato na matumizi sambamba na kurejesha nidhamu, uwajibikaji kwa watendaji wa serikali.

Mjumbe huyo alisema ukitaka kuleta maendeleo na kutimiza ilani ya uchaguzi ni lazima uanze na mambo makubwa matatu ikiwemo nchi kuwa na amani, utulivu na mshikamano.

Alisema hajawahi kuona wala kusikia kwamba kuna nchi yoyote duniani wameweza kuleta maendeleo huku kukiwa na vita na kusisitiza kuwa ikiwa nchi haina amani basi hakuna maendeleo yatakayoweza kupatikana.

“Hatuna haja ya kutizama nje tukatizama Congo, Somalia, Syria na Iraq, sisi wenyewe tujitizame ndani ya nchi yetu wakati tuliokuwa tuna mifarakano mikubwa kitu gani kilifanyika?”, alisema.

Alisema aliona ipo haja ya kudumisha amani kwa kulifanya hilo kwa kuzungumza na wenzao wa vyama vya upinzani ili kuunda serikali ya Umoja wa kitaifa ambayo lilikuwa ni takwa la kikatiba.

Dk. Mwinyi alisema hatua ya pili katika kuleta maendeleo ni kuwa na fedha kwani huwezi kujenga skuli, huduma za kiafya na maendeleo mengine bila ya kuwa na rasilimali hiyo.

Alisema kwa bahati mbaya ukusanyaji wa mapato ya serikali ni mbaya na fedha za serikali zinapotea hasa katika mashirika makubwa, kodi ndogo zinapotea kwa asilimia kubwa na kuishia mikononi mwa watu binafsi.

Dk. Mwinyi alisema pia katika matumizi pia kulikuwa na matatizo kutokana na fedha nyingi kutumika na hakioni kinachofanywa. “Zipo fedha zinazokwenda kwenye miradi ya maji, elimu, lakini huoni kinachofanyika ilinibidi nilisimamie hili kwa nguvu zangu zote kwani bila ya fedha huwezi kuleta maendeleo”, alibainisha.

Alibainisha kuwa anatambua fika Zanzibar ni ndogo na alitamka wazi kuwa ni lazima watu atawachukulia hatua na anaendelea katika jambo hilo ili wengi wapate manufaa.

Alisema wapo watu wanaodhani kuwa anawaonea watu na kubainisha kuwa hana sababu ya kumuonea mtu bali anataka kuleta nidhamu ya mapato na matumizi ya fedha za serikali.

Mbali na hayo alibainisha kuwa hatua ya tatu ni kuwajibika kwa watendaji wa serikali, hivyo ni lazima kila mmoja awajibike kwa nafasi yake kwani bila kuwajibika hawawezi kutekeleza ilani ya uchaguzi.

Dk. Mwinyi alisema katika kipindi cha miezi sita mambo hayo ndiyo aliyoanza nayo ili wakitoka hapo maendeleo makubwa yaweze kupatikana kwani wapo wanaojiuliza juu ya utendaji wake.

Dk. Mwinyi alisema katika kipindi hicho wameifanya kazi hiyo na kutengeneza maadui wengi kwa sababu tu ya kuwachukulia hatua watu waliothibitika kuchukua fedha za serikali.

“Najiuliza kila siku nnayoyafanya yana faida kwa nchi? nnayoyafanya yanawafurahisha wengi au wachache? na nikipata jibu yana faida na nchi na yanawafurahisha wengi, basi naendelea nayo”, alisisitiza.

Akizungumzia lengo la mkutano huo ni kutoa shukrani za dhati kwa viongozi hao na wanaCCM kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kipindi cha uchaguzi kwa kufanikisha ushindi wa asilimia 100.

Alisema, wanaCCM wamefanya kazi nzuri na ya kupongezwa kukipatia ushindi wa aina yake kwani haijawahi kutokea hivyo viongozi wote waliofanikiwa wana kila sababu ya kushukuru.

Alifahamisha kuwa serikali ina jukumu kubwa kwa wananchi kutokana na kuwaahidi mambo mbalimbali kupitia ilani ya CCM, hivyo deni hilo lazima litekelezwe na kuwataka wanaCCM waunge mkono hatua zinazochukuliwa ili 2025 chama hicho kishinde tena uchaguzi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini, Iddi Ali Ame, alisema walikula ahadi kutopoteza eneo lolote la uchaguzi katika kipindi cha uchaguzi kuanzia wadi na Jimbo.

Aidha alisema Mkoa wa Kaskazini kwa uchaguzi wa mwaka 2020 wamevunja rekodi ya kufikia asilimia 84 ya kura ukilinganisha na miaka yote ambayo walikuwa wakifikia asilimia 45 hadi 54 na kupoteza baadhi ya majimbo katika mkoa huo.

Akizungumzia suala la ripoti ya CAG walimuomba kiongozi huyo kuendelea na kasi yake ya kuwawajibisha wale wote watakaobainika kula fedha za wananchi na kuahidi kumuunga mkono kwa asilimia 100 katika kuwawajibisha watu hao.

Nao wanachama hao walimpongeza kiongozi huyo kwa kusimamia suala la uadilifu na uwajibikaji kwa watumishi wa umma hasa kitendo cha kuwawajibisha watu waliokula mali ya umma na kumuomba kuendelea na kazi hiyo ili Zanzibar iweze kufikia asilimia kubwa ya maendeleo.