NA MOHAMED HAKIM

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameagiza Vyuo Vikuu nchini kuandaa tafiti za kisayansi zinazohusiana na masuala ya uchumi wa buluu ili kuisaidia serikali kufikia malengo waliyojiwekea katika sekta hiyo.

Pia Dk. Mwinyi alivitaka vyuo hivyo kuanzisha fani zinazohusisha kada hizo ili kuinua uchumi wa Zanzibar na watu wake.

Dk. Mwinyi alitoa kauli hiyo katika hutuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Simai Mohammed Said, katika mahafali ya 18 ya Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU), Tunguu nje kidogo ya mji wa Unguja.

Alisema asilimia kubwa ya vijana wa Zanzibar ni zao la chuo hicho na vyuo vyengine kuangalia uwezekano wa fani zinazotolewa kuendana na mikakati na malengo ya serikali hasa katika kukuza uchumi wa nchi.

Alibainisha kuwa vyuo vikuu vinahitajika kuangalia zaidi kwenye masuala ya uvumbuzi na utumiaji wa malighafi za baharini kwa maslahi mapana ili kufikia lengo la uchumi wa buluu.

Aidha alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia ilani ya uchaguzi ya CCM imeahidi ajira 300,000, hivyo ana imani lengo hilo litafanikiwa ikiwa watafanya kazi kwa pamoja na vyuo vya amali na taasisi zote za elimu ya juu.

“Naamini kuwa mambo mengi yanahitaji kuangaliwa kwa makini ili kuhakikisha fani zinazotolewa katika chuo hiki zinaendana na agenda za serikali za maendeleo ili kunyanyua uchumi wa taifa letu,” alisema Dk. Mwinyi.

Hivyo alivitaka vyuo vikuu nchini kuangalia mambo kwa upana na kuishauri serikali hususani katika kipindi hiki cha mabadiliko ya kiuchumi.

Alisema vyuo vikuu vinaweza kuishauri serikali katika kutengeneza sera zilizo bora pamoja na kuboresha sheria ili kuleta sheria rafiki ambazo zitaweza kuisaidia serikali.

Hata hivyo, alivitaka vyuo vikuu vyote vitatu hapa nchini kutafuta njia ya kuanzisha mahusiano na Tume ya Mipango Zanzibar kwa lengo la kufahamu maeneo mapya yaliyowekwa na serikali ili kuwekeza na hatimae kukuza  maendeleo ya Zanzibar.

Dk. Mwinyi alisema anafuraha kuona vijana wa kizanzibar na mataifa mengine wanahitimu masomo yao katika chuo cha ZU jambo ambalo sio rahisi kama inavyoonekana.

Mapema Mkuu wa chuo hicho Mhandisi Dk. Abdullqadir Othman Hafiz, alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kuapishwa kuwa Rais wa Zanzibar na kukita katika kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.

Naye Makamu Mkuu wa chuo hicho Prof. Haruna Msubuga, alisema chuo hicho kimejipanga kutoa fani mpya zinazohusiana na masuala ya uchumi wa buluu na kuandaa tafiti zinazohusiana na masuala ya uchimbaji wa mafuta na gesi asilia.

Alibainisha kuwa tafiti nyengine zitahusiana na masuala ya uvuvi lengo na dhamira ni kuisaidia serikali ya Zanzibar kufikia malengo yake iliyojiwekea ya kuimarisha uchumi wa buluu na kutoa ajira kwa vijana.

Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) tangu kianzishwe takribani miaka 20 hivi sasa, kimehitimisha wanafunzi 11,355 katika kada mbalimbali ikiwemo wanawake 6,041 na wanaume 5,284 ambapo katika mahafali ya 18 mwaka huu wamehitimu jumla ya wanafunzi 842 katika fani tofauti ikiwa wanawake 332 na wanaume 510.