ZASPOTI
WIKI iliyomalizika ulimwengu wa soka uliingia katika malumbano makubwa baada ya klabu sita za Ligi ya kuu, kutaka kushiriki ligi kuu mpya.( Super League)
Manchester City ilikuwa ya kwanza kujiondoa baada ya Chelsea kuashiria nia ya kuandaa waraka wa kujiondoa.
Klabu za Arsenal, Liverpool, Manchester United na Tottenham pia zimefuata mkondo.
Klabu hizo ‘Sita kubwa’ za soka nchini Uingereza zilikuwa sehemu ya mashindano hayo, ambayo yanajumuisha Atletico Madrid, Barcelona na Real Madrid za Uhipania pamoja na AC Milan, Inter Milan na Juventus, za Italia, zilizotangaza mpango wa kuanzisha ligi nyingine, ambayo ingebuni mashindano ya katikati ya wiki.
Karibu mashabiki 1,000 walikusanyika nje ya uwanja wa Chelsea wa Stamford Bridge kabla ya mchezo wao dhidi ya Brighton siku ya Jumanne kupinga kujihusisha kwa klabu yao.
Makamu mwenyekiti mtendaji wa Manchester United Ed Woodward, ambaye alikuwa akihusika katika majadiliano ya Super League, ametangaza ataondoka katika nafasi yake mwishoni mwa 2021.
Wachezaji wanaoongoza katika baadhi ya klabu sita walionesha kutokubali kwao kuingia ligi hiyo mpya
Nahodha wa Liverpool Jordan Henderson alisema kwenye mitandao ya kijamii kwamba ni “msimamo wa pamoja” kwa timu yake kuwa hawataki Super League ifanyike.
Malumbano hayo yalizidi kukolea hadi pale mashiriki makubwa ya soka ulimwenguni ya FIFA na UEFA, kuingilia kati na FIFA kufikia hatua ya kutamka wazi kuwa wachezaji watakaoshiriki mashindano hayo watafungia kucheza kombe la dunia.
Rais wa Real Madrid, Florentino Perez, ambaye alitajwa kama mwenyekiti wa ESL, alisema mashindano hayo yalianzishwa “kuokoa soka” kwa sababu vijana “hawapendi tena” mchezo huo kwa sababu ya “mechi nyingi duni”.
Nimeamua kuzungumza kidogo jambo hili ili kuweka mfano wa mashindano mbali mbali ambayo yanafanyika hapa Zanzibar bila ya utaratibu na hakuna tija yoyote inayopatikana.
Mashindano hayo ambayo hapa Zanzibar tmeyapa jina maarufu ya (Ndondo), ambayo yamekuwa yakifanyika kila pembe ya Zanzibar, tena kushirikisha wachezaji wakubwa wanaoshiriki ligi kuu Zanzibar.
Hebu tuangalie mfano huu, kwa nini FIFA na UEFA ziliamua kuingilia kati suala hili na hata kufikia hatua ya kutamka wazi kuwa itamfungia mchezaji ambaye atashirikia mashindano hayo.
Hapa nataka kutoa rai kuwa umefika wakati sasa kwa ZFF nayo kujaribu kuiga mfano wa haya, kwa kuangalia faida na hasara ya kuwa na mashindano hayo, ambayo dhahiri kuwa FIFA imeona hakuna faida ya kuwa nayo.
Ni ukweli kuwa hapa Zanzibar yapo mashindano mengi ambayo yanafanyika na hayana maslahi hata kidogo kwa nchi na wachezaji wenyewe, lakini yamekuwa na nguvu kulinganisha na yale yenye sifa kubwa.
0774423007
binkhalidson@gmail.com