HIVI karibuni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi alifanya hafla ndogo, lakini ilikuwa maalum kwa umaalum wake ambapo aliwaalika viongozi, watendaji serikali na waandishi wa habari pale ikulu.

Hafla hiyo ilihusu kukabidhiwa ripoti iliyokamilika iliyotayarishwa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (CAG) kwa mwaka 2019/2020.

Kila mwaka moja ya jukumu la msingi la ofisi ya CAG ni kutayarisha ripoti hiyo, hata hivyo mwaka huu imekuwa kipekee kwa Dk. Mwinyi kuipokea hadharani na kubainisha kwa ufupi kile kilichobainika wakati wa ukaguzi.

Ripoti hiyo kubwa ina mambo mengi na imeangazia sehemu tofauti za kiutendaji serikalini, lakini kwa ufupi kabisa taarifa ya CAG ya mwaka 2019/2020 imeonesha udhaifu mkubwa uliopo katika taasisi zetu jinsi zisivyozingatia sheria na taratibu kwenye matumizi ya fedha za umma.

Kuna taasisi zimepata hadi chafu na zipo zilizopata hati zenye shaka, lakini pia ripoti imeonesha mambo yalivyokuwa hayakukaa sawa hasa kwa kukosekana kwa vielelezo vya matumizi ya fedha kwenye taasisi za serikali.

Kwenye miradi mikubwa ambayo tunaitegemea kuwa nguzo za kiuchumi kwa nchi yetu na kustawisha maendeleo ya wananchi ripoti imebainisha kuna mambo yasiyo ya kupendeza yamefanywa.

CAG ameonesha jinsi Zanzibar ilivyo na mifumo dhaifu inayotoa mwanya kwa wenye nia ovu kufanya vitendo vya kifisadi na uhujumu wa uchumi kwa faida zao binafsi.

Kibaya zaidi wapo waliomuona CAG kama adui anayehatarisha maslahi yao kwani walijaribu kumzuia asitekelezea majukumu yake, hili linashangaza kwa nini umzuie CAG asitekeleza majukumu yake kisheria?

Unapomzuia CAG asitekeleza majukumu yake ambayo yameainishwa kwenye katiba na sheria za nchi una lengo gani? Tukuelewe vipi? Lakini je wewe ni mkubwa kiasi gani katika nchi hii?

Tuseme tu hakuna haja ya kunyoosheana kidole kwa yale yaliyokuwemo kwenye ripoti za CAG, ila tunadhani viongozi na watendaji serikalini ripoti wamezisikia na bila shaka ni wakati wa kuangalia tunaanza vipi baada ya matokeo haya.

Itashangaza sana na kiukweli Rais wetu hatakuwa na sababu ya kuwaonea huruma viongozi na watendaji pale ukaguzi wa mwakani utakapo kuja kutoa matokeo kama ya mwaka huu bila ya kuonesha kuwepo kwa mababadiliko.

Tumshukuru sana CAG kwa kutuonesha wapi tulipoteleza, wapi tulijikwaa na wapi tulipoanguka, ni wakati wa kuangalia mbele kuwa na uzalendo wa kuipenda nchi yetu na sio kuendekeza maslahi binafsi.

Dk. Mwinyi aliingia na kauli mbiu ‘Yajayo ni neema tu’, lakini bila ya kila mmoja wetu kwa nafasi yake kutekeleza wajibu wake, neema hizo ambazo kila mmoja wetu angependa anufaike hatutazipata.

Ubinafsi na tamaa hazisaidii kujenga nchi yetu, kizazi kijacho cha kizanzibari kitafurahia maisha kama kila mmoja wetu atakuwa mzalendo na mwenye mapenzi katika kuijenga nchi.