KHAMIS AMANI NA ASYA HASSAN
JUMLA ya hekta 230 za miti aina ya mikoko na mikandaa imepandwa katika fukwe za Unguja na Pemba ili kudhibiti uingiaji wa maji chumvi katika maeneo ya kilimo na mabadiliko ya tabia nchi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Saada Mkuya Salum, aliwaambia Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi huko Chukwani, alipokuwa akijibu swali la Mwakilishi wa jimbo la Wingwi, Kombo Mwinyi Shehe.
Katika swali lake, Shehe alitaka kujua hatua zinazochukuliwa na serikali kupambana na tatizo la maeneo ya kilimo yanayotumiwa na wananchi kwa kujiletea maendeleo kuingia maji chumvi .
Akijibu swali hilo, Dk. Mkuya alifahamisha kwamba, serikali imechukua hatua mbali mbali za kupambana na hali hiyo kwenye mwambao wa ukanda wa pwani wa Unguja na Pemba kwa kupanda miti hiyo.
Alisema hatua hiyo imesaidia kupunguza athari zilizokuwa zikijitokeza katika maeneo ya kilimo, kwa lengo la kuwafanya wananchi waendelee kuyatumia kwa shughuli za kiuchumi.
Aliyataja baadhi ya maeneo yaliyopandwa miti hiyo kuwa ni Charawe, Ukongoroni kwa upande wa Unguja na Pemba ni katika eneo la Tumbe.
Sambamba na hatua hiyo, pia serikali imejenga matuta kwa baadhi ya maeneo ili kuzuia uingiaji maji ya bahari katika maeneo ya kilimo pamoja na kujenga kuta mbili zenye urefu wa mita 50 katika eneo la Kisiwa Panza, Pemba.
“Serikali kwa kutambua kwamba wakulima wameathirika kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, imechukua juhudi mbali mbali kuhakikisha wakulima wanajipatia njia mbadala ya kujipatia kipato, ikiwemo pamoja na kusaidia mizinga 350 na zana za kufugia nyuki kwa vikundi 36 Unguja na 20 Pemba,” alieleza Dk. Mkuya.
Alifahamisha kwamba, serikali itaendelea kuchukua juhudi zaidi katika kuimarisha maeneo ya kilimo yaliyoathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi na kuwapatia kazi mbadala za kuwaongezea kipato wananchi ili kuhimili mabadiliko hayo kupitia miradi ya maendeleo.