NA WAANDISHI WETU, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, ameupongeza uongozi wa jumuiya ya Taasisi za Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Tanzania (TAHLISO) unaomaliza muda wake kwa mafanikio waliyoyapata katika kusaidia maendeleo ya wanafunzi vyuoni.

Hemed alieleza hayo jana alipozungumza na viongozi wa taasisi hiyo wanaomaliza muda na kuwatambulisha viongozi wapya waliochaguliwa wakati walipofika ofisini kwake Vuga jijini Zanzibar.

Alisema mashirikiano waliyoyaonyesha kati yao na viongozi wa vyuo pamoja na serikali yameisaidia sana serikali kutatua changamoto zinazowakabili wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu nchini akitolea mfano suala la upatikanaji wa mikopo ya elimu ya juu.

Hemed aliwasihi viongozi hao kuendeleza ushirikiano kati yao ili taifa liweze kupata maendeleo zaidi hasa katika sekta ya elimu na kuwaeleza kuwa serikali inawaamini vijana kwa mchango wao wanaoutoa katika kufanikisha maendeleo ya taifa.

Makamu wa Pili, aliwaasa viongozi wapya wa taasisi hiyo waliochaguliwa, kujenga uzalendo na kuachana na muhali katika uwajibikaji wao kwa kuunga mkono jitihada za viongozi wa serikali hasa kwenye kupiga vita rushwa, ubadhirifu, uzembe, uhujumu wa uchumi mambo ambayo yanazorotesha ufanisi katika majukumu yao.

Kuhusu elimu nchini, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema serikali inatambua umuhimu wa uwepo wa vyuo vikuu kwa kutambua kuwa ni eneo muhimu lenye mchango mkubwa zaidi kwa maendeleo ya taifa.

Aliwataka viongozi hao kuendelea kueleza mema yanayofanywa na serikali zote mbili, ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, akitolea mfano kuhubiri faida za Muungano wa Tanzania ulioasisiwa tangu mwaka 1964.

Hemed aliwahakikishia viongozi hao kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo tayari kutoa mashirikiano na kuwaeleza kuwa inafurahishwa kuona taasisi mfano wa hizo zikiwajibika vyema na kuwataka wasisite kuomba ushauri kutoka serikalini pale watakapohitaji.

Mapema Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Ndugu Peter Josphet Niboye amempongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa jitihada zake anazozichukua katika kukuza elimu nchini pamoja na msimamo wake dhidi ya kupiga vita vitendo vya udhalilishaji.

Akigusia suala la mafanikio ya taasisi hiyo, Ndugu Niboye amesema katika kipindi cha uongozi wao wamefanikiwa kutatua changamoto mbali mbali za wanafunzi huku wakihubiri suala la amani, utulivu na kuondosha migomo ya wanafunzi hali iliyosaidia kwa kiasi kikubwa kuendelea kupatikana kwa utulivu vyuoni.

Uongozi wa jumuiya ya taasisi za wanafunzi wa elimu ya juu Tanzania, wamekuwa wakishirikiana na taasisi mbali mbali za serikali, tokea kuasisiwa kwake.