NA KHAMISUU ABDALLAH, MOHAMMED RASHID (DOMECO)

WIZARA ya Fedha na Mipango Zanzibar, imesema mapato ya Muungano yanayokusanywa Zanzibar huwekwa katika mfuko Mkuu wa Hazina wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kutumika kugharamia mambo yasiyo ya Muungano kwa Zanzibar.

Kwa upande wa mapato ya Muungano yanayokusanywa Tanzania bara huwekwa katika mfuko Mkuu wa Hazina wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na kutumika kugharamia mambo ya Muungano na yasiyo ya Muungano kwa Tanzania bara kutokana na kutofikiwa uamuzi wa kugawana mapato hayo.

Waziri wa Wizara hiyo Jamal Kassim Ali, alitoa kauli hiyo wakati akijibu suala la msingi liloulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Amani, Rukia Omar Ramadhan alietaka kujua kuna mapendekezo na kushauri gani ambao upo kisheria kuhusu Uhusiano wa kifedha baina ya pande zote mbili za SMT na SMZ.

Alisema tume  ya pamoja ya fedha imeandaa na  kuwasilisha kwa SMT na SMZ mapendekezo na ushauri kuhusu vigezo vya kugawana mapato ya Muungano na kuchangia gharama za Muungano ambapo pande zote mbili za Muungano zinaendelea na mashauriano.

Alibainisha kuwa uamuzi utakapofikiwa na pande zote mbili za Muungano utaratibu wa kudumu wa kugawana mapato ya Muungano na kuchangia gharama za Muungano utaanza kutumika rasmi.

Aidha, alisema kwa sasa kila upande wa Muungano umeendelea kunufaika na mapato yanatokana na misaada na mikopo kutoka kwa washirika wa maendeleo pamoja na gawio la Benki Kuu ya Tanzania kwa uwiano wa asilimia 4.5 kwa SMZ na asilimia 95.5 kwa SMT.

Hata hivyo, alibainisha kuwa serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, imekuwa inarejesha mapato ya kodi yatokanayo na mishahara ya watumishi (PAYE) wa Muungano wanaofanya kazi upande wa Zanzibar.

Sambamba na hayo alibainisha kuwa mapitio ya mfumo unaopendekezwa na tume ya pamoja na Fedha utafanyika  baada ya pande mbili kuridhia mapendekezo ya tafiti zilizowasilishwa na tume hiyo iliyoundwa na hatimae kufikia uamuzi wa pamoja na mfumo huo kuanza kutumika hususan suala hilo ambalo ni matakwa ya kikatiba.

Akizungumzia kuanzisha kwa tume hiyo alisema  imeanzishwa kupitia ibara  ya 134 ya katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na sheria ya Tume ya pamoja ya fedha sura 140.

Aidha alisema majukumu ya  Tume yameainishwa katika ibara ya 133 na 134 ya Katiba ambapo kwa mujibu wa sheria tume hiyo ina jukumu la kutoa mapendekezo na ushauri kuhusu Uhusiano wa kifedha Kati ya SMZ na SMT.

Nae, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi  Dk. Khalid alisema kulikuwa na  hoja 25 za Muungano Kati ya hizo hoja 15 zimeshapatiwa ufumbuzi na hoja 10 zinaendelea kutafutiwa ufumbuzi.

Alisema kamati inayoratibu masuala ya Muungano sekretariet yake tayari imeshakaa hivi karibuni kwa pande zote mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania zinazoongozwa na makatibu wakuu na karibu wataitisha vikao vya mawaziri wanaohusika na sekta hiyo.

Dk. Khalid alisema pia kutafanyika kikao kikubwa cha kamati itayoongwa na Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaaliwa Majaliwa na kuahidi kuwa jambo hilo litapatiwa ufumbuzi katika vikao hivyo.