JUBA, SUDAN KUSINI

SUDAN Kusini imesema ina dozi zaidi ya 126,000 za chanjo ya virusi vya corona za AstraZeneca kutokana na idadi ndogo ya watu waliojitokeza kupata chanjo hiyo.

Kwa mujibu wa wizara ya afya nchini humo watu waliopatiwa chanjo ni 6,403, zoezi lilioanza mwezi Aprili mwaka huu.

Wizara hiyo imesema kuwa lengo la nchi hiyo ni kutoa chanjo kwa watu milioni 2.4 kati ya idadi ya watu milioni 12 nchini humo.

Mnamo Machi 25 mwaka huu, Sudan Kusini ilipokea dozi 132,000 za chanjo ya virusi vya corona ya AstraZeneca kutoka COVAX na inatarajia kupokea jumla ya dozi 732,000 za chanjo hiyo ndani ya miezi sita ya mwanzo ya mwaka huu.

Msimamizi wa kamati ya kukabiliana na corona iliyo chini ya wizara ya Afya nchini humo Richard Lako alisema wizara hiyo imeamua kuongeza vituo vya kutoa chanjo hiyo mpaka kufikia 23 katika mikoa 10 ya nchi hiyo.

Lako alisema kuongezwa kwa vituo hivyo kunatoa nafasi kwa wananchi kuitikia wito na kujitokeza kupatiwa chanjo za kukabiliana na ugonjwa huo.

Katika hatua nyengine nchini humo mratibu wa mambo ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, Alain Noudehou amelaani mauaji ya mfanyakazi wa misaada kwenye kaunti ya Budi mkoani Ikweta ya Mashariki, Sudan Kusini.

Noudehou alisema mfanyakazi mmoja aliuawa wiki iliyopita wakati wahalifu walipofyatulia risasi gari la misaada ya kibinadamu lililokuwa likisafiri kwenda kwenye kituo cha afya.

Noudehou alizitaka serikali na jamii za Sudan Kusini zihakikishe wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu wanaweza kupita salama barabarani na kutoa msaada kwa watu waishio katika mazingira magumu nchini humo.