NA ZUHURA JUMA, PEMBA

USTAHAMILIVU wa kisiasa ni jambo muhimu katika jamii ambalo ndani yake huzaa amani, upendo na utulivu kwa wanajamii.

Mfano wa hilo ni kwamba, viongozi wangekuwa na ustahamilivu na uvimilivu, siasa isingekuwa chungu mithili ya shubiri hasa katika bara la Afrika.

Yapo mataifa mengi duniani sasa yamerudi nyuma baada ya kukosekana kwa uvumilivu wa kisiasa, watu hufarakana na kisha kuzaa mapigano.

Kukosa uvumilivu mataifa mengi huingia katika machafuko na kusababisha vifo, watu hukosa makaazi na wengine kuhamia nchi nyengine wakiwa wakimbizi.

Ingawa kwa Tanzania bado viongozi wa vyama vya siasa wamejengwa na uvumilivu wa kisiasa, jambo linalopelekea kufarakana na kisha kuelewana.

Imani ya dini, uvumilivu wa kuzaliwa, utamaduni wa kuhurumiana, na udugu wa kuzaliwa kwa jamii ya Tanzania na Zanzibar, siasa hufanyika na kupita bila ya kuacha madhara makubwa.

HALI YA ZANZIBAR KISIASA NA UVUMILIVU

Zanzibar ambayo iliingia kwenye mfumo wa vyama vingi tangu mwaka 1992, historia ya uvumilivu na utamaduni wa kuhurumiana ndipo ilipo anzia.

Utamaduni na hamu ya kuingia ikulu kwa kila mwanasiasa kwenye uchaguzi mkuu kwa chaguzi kadhaa zilizopita, kamwe haikuiweka Zanzibar ikiwa salama na kupelekea siuntofamu za hapa na pale.

Kwa wakati huo maridhiano kadhaa yalifanywa hapa Zanzibar, lengo likiwa ni kuwaweka pamoja wananchi wa Zanzibar ambao asili yao ni udugu.