NA ASIA MWALIM

JAMII nchini imeshauriwa kuwa na utamaduni wa kusaidiana kwa hali na mali ili kuimarisha mahitaji ya watu wasiojiweza.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud aliyasema hayo alipokua akikabidhi misaada ya vyakula mbalimbali kwa familia 100 zinazoishi katika mazingira magumu huko Matwemwe wilaya ya Kaskazini Unguja.

Alisema endapo watajitokeza wafadhili wenye lengo la kuboresha maisha ya watu wenye mazingira magumu na uhitaji wa vitu muhimu itaweza na kuwapunguzia ukali wa maisha.

Aidha alisema kuwepo kwa utamaduni wa kusaidiana kutengeneza  upendo wenye nia thabit kati ya mtoaji na mpokeaji sadaka ambapo ni adimu kupatikana.

Alisema lengo la msaada huo ni kuimarisha hali za wanyonge, kubadilisha maisha ya watu ili wajikimu kwa  kuweza kupata vyakula vitakavyo wasaidia kwa ajili ya futari.

Alisema atahakikisha msaada huo unafika kwa walengwa kama maagizo ya watoaji walivyoeleza, hivyo atahakikisha kila mwenye vigezo ataweza kupata chakula hicho.

Aidha katika hatua nyengine alifanikiwa kukabidhi mabati 5 kwa familia moja ambayo iliomba hifadhi hiyo, baada ya kuvujiwa kwa muda ambapo, bati hizo zilitolewa na Mwakilishi wa Jimbo hilo.

Alisema viongozi wa mkoa huo wapo katika harakati za kufanikisha mahitaji ya wanakijiji hicho ikiwemo kuimarisha  makaazi yao na kujenga vyoo vya kisasa.

Akitoa shukrani kwa Mkuu wa Mkoa, kwa niaba ya wenzake Rashid Mussa Mbaraka ameshukuru kupatiwa msaada huo na kuwaomba wafadhilii wengine kujitokeza kusaidia kwa namna nyengine.

Alisema baadhi ya watu wanashindwa kutimiza mahitaji yao ya kiuchumi kutokana na ujira mdogo wanaopata katika harakati zao.

Katika hafla hiyo, Ayoub alikabidhi msada huo uliotolewa na wahisani wa ndani na je ya Zanzibar ambao hawakutaka kutajwa majina ikiwa ni sehemu ya sadaka ya  Mwezi mtukufu wa Ramadhan ambapo tende katuni15 na mchele vipolo 100 vyenye uzito wa kilo kilo 25 vilikabidhiwa.