NA BAKAR MUSSA, PEMBA

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Richard  Tadei Mchomvu, amewaomba Masheha na Wasaidizi wa Sheria  Wilaya ya Chake Chake, kumpa ushirikiano ili kuendelea kuwalinda wananchi na mali zao, ikiwa ndio lengo la kuwepo Jeshi hilo kwani wanahaki ya kubaki wakiwa salama.

Hayo aliyaeleza huko katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Kusini Pemba, wakati alipokuwa akijitambulisha kwake kwa Masheha na wasaidizi wa Sheria  Wilaya ya Chake Chake kufuatia mabadiliko yaliotokea hivi karibuni ya uteuzi wa Kamanda huyo.

Alieleza kuwa Masheha ndio viongozi wa mwanzo wa Serikali na waliokaribu na wananchi ambao miongoni mwao ndipo wanakotoka wahalifu hivyo ni vyema kuwa tayari  kutowa ushirikiano kwa jeshi hilo, ili kuondowa matatizo yanayoikumba jamii .

“ Nyinyi Masheha sio watu wa kuombwa ni wajibu wenu kushirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha wananchi wanaishi katika hali ya amani na utulivu huku  wakiendelea na shuhuli zao bila ya bughudha yoyote,”alisema Kamanda huyo.

Aidha, aliwataka Masheha kufichuwa maovu yote yaliomo ndani ya jamii wanazoziongoza ikiwemo, Udhalilishaji wa kijinsia, wizi wa mazao ,mifugo  na  hata kuwafichuwa watendaji wake ambao lugha zao kwa wananchi pale wanapokwenda kuwalalamikia matatizo yao sio mzuri.

Kamanda alisema kumekuwa na matendo mengi maovu ya udhalilishaji ,wizi wa mazao na mifugo, lakini baadhi ya Masheha wamekuwa wakikaa kimya hawaripoti wanabakia wakitembea mitaani bila kulifanyia kazi tatizo hilo wasione kufanya hivyo ni ufahari ni kutowajibika.

Alisema kuna uwezekano wako baadhi ya watendaji wake wanapopelekewa malalamiko na wananchi wamekuwa na lugha mbaya, na hivyo kuwafanya walalamikaji kulichukia Jeshi, hilo na kusema hawatokwenda tena kuripoti matatizo yao hilo likitokea wamwambie yeye .

“ Mimi niwatowe hofu Masheha na wananchi niko tayari kupokea na kusikiliza malalamiko yenu na wananchi munao waongoza pale likitokea tatizo kutoka kwa watendaji wangu kama vile dharau na kauli mbaya , nawaomba muniambie kwani bila ya kufanya hivyo sitojuwa mutabaki kulalamika mahali pasipo sahihi,”alieleza.

Alifahamisha kuna matatizo yanatokea ndani ya Shehia pengine na Polisi yuko anayaona na hachukuwi hatuwa pengine kwa ujamaa wa mmoja kati ya waliosababisha tatizo hilo, likitokea apatiwe taarifa yeye au OCD.

“ Tunataka sisi tuwaamini na nyinyi muliamini Jeshi letu na tuendelee kushirikiana, ili wananchi waweze kupata haki zao na waache kulilamikia Jeshi letu naomba tushirikiane,”alisisitiza.

Hivyo alisema Jeshi la Polisi, haliwezi kufanya kazi zake ipasavyo iwapo litakosa ushirikiano wa dhati kutoka kwa Masheha ambao wako karibu na jamii na wanawaelewa miongoni mwa watu wakorofi.