Yatahadharisha wimbi la tatu kuipiga Tanzania

NA MWANDISHI WETU

KAMATI ya kitaaluma iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, kutafiti juu ya mwenendo wa ugonjwa wa corona jana imewasilisha rasmi ripoti yenye mapendekezo 20 ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Kamati hiyo iliwasilisha ripoti kwa Rais Samia, ambapo ilifanyia kazi hadidu rejea 12 zilizohusu maeneo mbalimbali ya tathmini ya mwenendo wa ugonjwa na hatua za udhibiti ikiwemo chanjo hapa nchini, kikanda na kimataifa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Prof. Said Aboud alisema tangu kuingia kwa janga la ugonjwa huo, mnamo mwezi Machi mwaka jana, Tanzania imekumbwa na mawimbi mawili makubwa na kuna tishio la kutokea kwa wimbi la tatu la ugonjwa wa corona.

Kuhusu mapendekezo ya kamati hiyo baada ya kufanya tathimini ya ugonjwa huo inapendekezwa serikali ihuishe mipango ya dharura kwa ngazi zote kwa ajili ya kukabiliana na majanga likiwemo janga la ugonjwa wa corona.

Prof. Aboud alisema serikali itoe taarifa juu ya uwepo wa ugonjwa wa corona na ichukue hatua madhubuti kuimarisha hatua zote za afya za kinga (interventions) katika ngazi zote ili kuepusha wimbi la tatu la ugonjwa huo.

Alisema pendekezo jengine ni wataalamu wa afya watimize wajibu wao kitaalamu, kwa kuzingatia weledi, miiko na maadili katika kuelimisha, kukinga na kutibu ugonjwa wa corona nchini na nchi ishiriki katika maamuzi na itekeleze maazimio ya kikanda na kimataifa iliyoridhia katika jumuiya za EAC, SADC, AU na WHO.

Kuhusu chanjo dhidi ya ugonjwa wa corona, kamati inashauri serikali kwa kutumia vyombo vyake iendelee na hatua kuelekea kuruhusu matumizi huru ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa corona kwa kutumia chanjo zilizoorodheshwa na Shirika la Afya Duniani.

Pamoja na mapendekezo haya, Kamati Huru ya Kitaifa ya Ushauri wa Chanjo (NITAG) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ziendelee kushirikishwa katika kutoa ushauri na kudhibiti chanjo hizo; Kipaumbele cha utoaji wa chanjo dhidi ya corona nchini kwa kuanzia kiwe katika makundi yafuatayo kwa umuhimu:

Aidha wahudumu katika vituo vya kutolea huduma za afya na watumishi walio katika mstari wa mbele wa utoaji wa huduma (frontline workers) mathalani watumishi sekta ya utalii, hoteli, mipakani, viongozi wa dini na mahujaji, wazee na watu wazima kuanzia umri wa miaka zaidi ya 50, watu wazima wenye maradhi sugu mengine mathalani kisukari, shinikizo la damu, maradhi ya mfumo wa upumuaji, magonjwa ya figo.

Kamati imependekeza kufanya uhamasishaji na maandalizi ya upokeaji, utunzaji, usafirishaji na utoaji wa chanjo na wananchi wawe huru kuamua kuchanja na serikali iratibu upatikanaji wa chanjo kwa watumishi wa taasisi za kimataifa walioko nchini.

“Kamati imependekeza serikali ya Tanzania mpango wa COVAX kwa kuwasilisha andiko la kupatiwa chanjo, kwa kutumia fursa inayotolewa na GAVI, Serikali itumie fursa zilizopo wakati huu wa janga la COVID-19 kuanza mchakato wa uanzishaji wa viwanda vya kutengeneza chanjo”, alieleza Prof. Aboud.

Kamati hiyo imependekeza wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ikamilishe muongozo mpya wa matibabu ya ugonjwa wa COVID-19, na iendelee kuhakikisha kuwa matumizi ya tiba asili na tiba mbadala katika mfumo rasmi wa tiba za kisasa yanazingatia misingi ya kisayansi,

Prof. Aboud alisema serikali iendelee kutoa fursa na kuwawezesha wanasayansi kufanya tafiti kwa kufuata miiko, maadili na taratibu zilizowekwa ili kuimarisha kinga, tiba, uchunguzi wa ugonjwa wa COVID-19 na athari zake katika jamii nchini.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo Prof. Aboud amesema kamati hiyo  inapendekeza pia serikali iendelee kuzingatia mazingira ya kitanzania katika udhibiti wa ugonjwa wa COVID-19 katika kuamua kuweka au kutokuweka shuruti ya kujifungia (lockdown) na kuwa na ubunifu ili kuruhusu ukuaji wa uchumi na kuimarisha sekta zinazochangia katika uchumi.

Pendekezo jengine ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ziendelee kushirikiana ipasavyo katika hatua zote za kukabiliana na janga la COVID-19 pamoja na majanga mengineyo ikiwemo utoaji wa nyaraka za kimataifa kama vile Travel Advisory Note na Idara ya Maafa.

Aidha kamati hiyo imependekeza serikali iendelee kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, wadau wa maendeleo, sekta binafsi na vyombo vya habari katika mapambano dhidi ya janga la ugonjwa wa COVID-19.