NAIROBI, KENYA

WATU waliopata chanjo ya ugonjwa wa corona ya AstraZeneca nchini Kenya watalazimika kusubiri zaidi kupata dozi ya pili, kufuatia nchi hiyo kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chanjo hiyo.

Watu waliopata dozi ya kwanza, walitarajiwa kupokea dozi ya pili mwezi Juni, hata hivyo kutokana na uhaba wa chanjo hiyo watu hao watalazimika kusubiri.

Kwa mujibu wa taarifa uhaba wa chanjo hiyo unatokana na India ambayo ni mzalishaji mkubwa wa AstraZeneca, imesitisha usafirishaji wa chanjo hiyo kufuatia ongezeko la maambukizi katika nchi hiyo.

Wizara ya Afya nchini Kenya inasema, inaweka mikakati ya kupata chanjo nyingine kwa ajili ya watu wake, hali ambayo inazua wasiwasi nchini humo.

Enock Ocholla, ni miongoni mwa watu waliopewa dozi ya kwanza nchini humo, ambaye alisema huenda akapatwa na matatizo mwilini iwapo atakosa chanjo ya pili.

“Kwa mfano mimi nilipata chanjo ya kwanza tarehe moja mwezi Aprili na nilikuwa natarajia chanjo ya pili leo, lakini tunaelezwa kuwa chanjo zimekwisha mambo haya”, alisema Enock Ocholla.

Kenya ilipokea chanjo zaidi ya milioni moja mwezi Machi na licha ya kuanza kutolewa, baadhi ya Wakenya bado hawana imani na chanjo, licha ya elimu inayotolewa.

“Sina imani na chanjo zilizoidhinishwa nchini Kenya, najipa muda kidogo niweze kuona yale madhara yatakayotokana na chanjo hii, ndio niweze kuendea,” amebainisha Angose Philip.

Naye Victor Onyino, mtalaam wa afya nchini Kenya, alisema ni muhimu kupata dozi ya pili ya chanjo.

Chanjo kwa mara ya kwanza inaweza kutuzuia kupata janga la corona kwa asilimlia 80 na unapopata chanjo ya pili, huwa muhimu kwani ina maanisha kwamba inaongezea uwezo wake wa kuzuia kupata janga la corona kwa hadi asilimia 90.