NA KHAMIS AMANI

MUSSA Chande Jape (52) mkaazi wa Mtoni Kidatu wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja, Juni 28 mwaka huu anatarajiwa kufikishwa tena mahakamani, kuendelea na kesi ya shambulio la hatari inayomkabili.

Mshitakiwa huyo anayetuhumiwa kumshambulia Muki Makame Ussi, atafikishwa mbele ya Hakimu Makame Mshamba Simgeni wa mahakama ya mkoa Vuga, kuendelea na kesi hiyo.

Katika kikao kilichopita, kesi hiyo iliahirishwa kutokana na Hakimu huyo kuwa likizo, ambapo upande wa mashitaka chini ya Wakili wa serikali Asma Juma Khamis, kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), umeomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kutajwa.

Katika kesi hiyo, mshitakiwa huyo ameshitakiwa kwa kosa la shambulio la hatari, kinyume na kifungu cha 208 cha sheria namba 6/2018 sheria za Zanzibar.

Aprili 1, 2019 majira ya saa 1:30 za asubuhi huko Mtoni Kidatu wilaya ya Mjini mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, bila ya halali alidaiwa kumshambulia kwa kumpiga Muki Makame Ussi sehemu za kichwani na mikononi na kumsababishia kupata majeraha na maumivu makali mwilini mwake.