RAMALLAH, PALESTINA

KIJANA wa Kipalestina mwenye umri wa miaka 16 aliuawa kwa kupigwa risasi usiku wa kuamkia jana na wanajeshi wa Israeli karibu na mji wa Nablus kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi, madaktari na mashuhuda wa walisema.

Wizara ya Afya ya Palestina ilisema katika taarifa kwamba kijana huyo aliuawa wakati wa mapigano kati ya waandamanaji wa Palestina na wanajeshi wa Israeli katika kijiji cha Oudla, kusini mwa Nablus.

Wizara hiyo ilisema kijana mwingine wa Kipalestina alipigwa risasi na kujeruhiwa na wanajeshi wakati wa mapigano hayo hayo, na kuongeza kuwa yuko katika hali ya wastani.

Wakati huo huo, mashuhuda walitoa taarifa ya tukio hilo, walisema Nablus na vijiji kadhaa vya karibu vimekuwa vikishuhudia maandamano ya kila siku na mapigano kufuatia uvamizi wa jeshi la Israeli katika nyumba za Wapalestina katika eneo hilo.

Jeshi la Israeli limekuwa likitafuta watu wenye silaha wa Kipalestina ambao walifyatua risasi siku tatu zilizopita kwenye gari la Israeli na kuwajeruhi Waisraeli watatu. Hakuna mtu aliyedai kuhusika na shambulio hilo la risasi.