NA MWAJUMA JUMA
MCHEZAJI wa zamani wa Pamba FC Yussuf Selemani Matimbwa amesema mpira wa Zanzibar umekufa ikilinganishwa na zamani.
Mchezaji huyo aliyasema hayo hivi karibuni alipokuwa visiwani Zanzibar katika ziara ya kimichezo, akiwa na timu ya Chanika Veteran ambao walicheza mechi kadhaa za kirafiki.
Alisema pamoja na mambo mengine lakini mpira huo unaonekana kufa kutokana na kukosekana kwa ushindani wa wachezaji katika klabu ambazo zinashiriki ligi visiwani hapa.
Alisema ili mpira upande lazima ucheze na watu uliowazidi kiwango ili kupata hamasa ya kuwa vizuri na kusajili wachezaji wenye viwango.
Alisema wakati wa michuano ya kombe la Muungano aliziona timu za Zanzibar kuwa na uwezo mkubwa, lakini kwa sasa zipo chini kwa kukosa ushindani.
“Ili mpira uwe juu lazima ucheze na timu ambazo wachezaji wake wamekuzidi uwezo, sasa mnapokutana wenyewe kwa wenyewe mnazidi kuwa dhaifu na wenzenu wakiwa juu wanazidi kuwa juu”, alisema.
Matimbwa ambae pia alizichezea timu za Mbaramiguu Yanga, Maji maji na CDA alisema anaifahamu Zanzibar wakati alikupokuwa akishiriki kombe la Muungano, ambapo mpira ulikuwa katika kiwango kikubwa tofauti na sasa,ambapo kiwango kimeshuka.
“Kwa mfano timu ya Malindi ya zamani ilikuwa na wachezaji mpaka kutoka Zambia, kwa maana hiyo inaonekana huko nyuma walikuwa wanahitaji kitu fulani vipatikane ndani ya Zanzibar na kweli vilionekana na kuonekana timu zipo vizuri”, alisema.
Alifahamisha kwamba hali hiyo si kwa Malindi pekee bali hata kwa timu kama Small Simba, ambayo nayo ilisajili mchezaji kutoka Tanzania bara kwa hali yoyote.
Sambamba na hayo alisema wakati akiwa mchezaji kwenye michuano hiyo ya kombe la Muungano, aliwahi kucheza na timu za Malindi, Miembeni na Kikwajuni, ambazo ndio timu zilizokuwa wapinzani wao sana kwa kipindi hicho wakikutana nazo.