NA VICTORIA GODFREY
TIMU ya Kim Canteen imefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya ligi ya Vijana chini ya umri wa miaka 20 wilaya ya Kigamboni, inayoendelea kwenye uwanja wa skuli ya Msingi Kigamboni ,Dar es Salaam.
Timu hiyo ilipata nafasi ya kufuzu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kibada Rangers, katika mchezo wa hatua ya robo fainali uliochezwa Mei Mosi kwenye uwanja huo.
Dakika ya 12 Kim Canteen ilianza kupata bao la kwanza lililofungwa na Miquissone Michael,kabla ya Kibada kusawazisha dakika ya 30 likifungwa na Said Mkonde na Ogyen Sanga aliongeza bao la pili Kim Canteen dakika ya 65.
Akizungumza na Zanzibarleo kocha wa Kibada Athuman Shabani,alisema wanamshukuru Mungu kwa mchezo umeisha salama na vijana walipambana licha ya kupoteza mchezo wao.
Aliwapongeza wapinzani kwa kufuzu hatua hiyo sambamba na waandaaji wa ligi hiyo ambayo imewapa changamoto na kwenda kujipanga kwa msimu ujao.
” Niwashukuru wachezaji wangu walicheza kwa nidhamu na kupambana ili kupata matokeo mazuri lakini bahati haikuwa kwetu na wapinzani wetu wamefuzu hili tunawapongeza sana kuwatakia kila la heri kwa hatua inayofuata,” alisema Shabani.
Naye Mjumbe wa Kamati ya Soka la Vijana na wanawake wa Chama cha Soka Wilaya ya Kigamboni (KDFA) Neema David,alizipongeza timu hizi kwa kuonyesha mchezo mzuri na kuzitaka kujipanga kwa bidii.
” Niipongeze iliyoshinda na isiyoshinda ,lakini safari inaendelea ,hivyo walioshinda mkajipange kwa mchezo unaofuata pamoja hawakupata nafasi waende kujipanga upya kwa msimu ujao,” alisema Neema