NAIROBI, KENYA

TAARIFA Kutoka nchini Kenya zinaeleza kuwa kirusi cha corona cha India tayari kimegunduliwa katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Daktari Rashid Aman kutoka wizara ya afya nchini Kenya, amethibitisha kuwa kirusi cha corona cha India kimeingia nchini humo ambapo zaidi ya watu 15 wamepimwa na kubainika kuambukizwa.

“Wiki iliyopita tumechukua sampuli za wasafiri wanaotoka India na kuingia hapa nchini tumebaini kwamba kirusi cha corona cha India kimeingia nchini kwani tumebaini watu zaidi ya 15 wameambukizwa”, alisema Dk. Aman.

Kirusi hicho cha B.1.617 ambacho kinajulikana kama kirusi cha India, kimesababisha maafa makubwa nchini India ambapo kiasi cha watu milioni 20 wameambukizwa.

Kwa mujibu wa watalaamu wa afya wanaeleza kuwa kirusi hicho kinasambaa kwa haraka sana kuliko virusi vya aina nyengine vya corona vilivyowahi kugunduliwa.