NA MWAJUMA JUMA

KMKM imetwaa ubingwa wa ligi kuu ya Zanzibar msimu wa mwaka 2020 -2021, baada ya jana kushinda bao 1-0 dhidi ya Polisi katika mchezo uliochezwa uwanja wa Amaan.

Kwa ushindi huo KMKM inafikisha pointi 40 ambazo hazitakifikiwa na timu yoyote zilizokaribu nae.

Kwa mujibu wa msimamo wa ligi hiyo timu ambazo zinaifuata ni KVZ yenye  pointi 33,  Mafunzo na Zimamoto wana pointi 32 na kila mmoja imebakiwa na michezo miwili ambayo hata wakishinda hawatoweza kuzifikia.

Alikuwa mchezaji Mohammed Saidi  Mohammed aliiandikia bao timu yake hiyo  katika dakika ya 10 za mchezo huo na kuwafanya waondoke na pointi tatu.

Bao hilo ambalo lilionekana kuwatia ari ya kushambulia washambuliaji wa Polisi lilifanikiwa kudumu hadi mapumziko.

Katika kipindi cha kwanza Polisi walikosa nafasi nyingi za wazi, nafasi ambazo watapaswa kujilaumu.

Dakika na sekunde ziliendelea kuyoyoma na miamba hiyo kuzidi kushambuliana lakini hadi mwamuzi wa mchezo huo Issa Haji anapuliza kipenga ushindi ukaangukia kwa KMKM.

Aidha katika uwanja wa Mao Zedong A mchezo kati ya Zimamoto na KVZ ulimalizika kwa sare isiyokuwa na mabao.

Matokeo ya mchezo huo yanaifanya KVZ kufikisha pointi 33 na kuendelea kudima katika nafasi ya pili wakati Zimamoto anakuwa wa tatu akiwa na pointi 32.

Itakumbukwa kwamba katika mchezo wa awali timu hizo zilipokutana Polisi ilishinda mabao 2-1.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena Juni 1 mwaka huu ambapo katika uwanja wa Amaan JKU itacheza na Hard Rock na katika uwanja wa Mao Zedong A Polisi itakuwa uso kwa uso na Mlandege.