ZIMESHAPINDUKIA siku 10 tangu mzozo uliosababisha vita baina ya Palesrina na Israel ulipoanza, ambapo huko mjini Gaza mashambulizi ya anga yanayofanywa na Israel yamesababisha uharibifu mkubwa.
Kila asubuhi jua lilipochomoza wakaazi wa mji wa Khan Younis wanapekua vifusi pamoja na mabaki ya nyumba za familia ambazo zimeharibiwa kabisa kutokana na mashambulizi ya anga yanayofanywa na jeshi la Israel.
Taarifa zinaeleza kuwa tangu kuanza kwa mapigano hayo Wapalestina 230 wameuwawa ikiwemo watoto 65 na wanawake 39 na wengine zaidi ya 1,710 wamejeruhiwa.
Aidha Wapalestina wengine 58,000 wameyahama makaazi yao kukimbia hujuma za ndege za Israel au baada ya nyumba zao kuharibiwa.
Netanyahu waziri mkuu wa Israel anayechukulia vita hivyo kama mtaji wa kisiasa, amekataa katakata wito wa Rais Joe Biden wa kusitisha mapigano ambayo yamesababisha vifo vya mamia ya watu.
Ni mara ya kwanza kwa washirika hao wawili kutofautiana hadharani tangu kuanza kwa mapigano hayo hilo linaweza kutatiza juhudi za kimataifa za kutaka kusitishwa kwa mapigano.
Pamoja na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kumaliza mkutano wake wa dharura kuhusu mzozo huo, wanachama 15 hawakufikia makubaliano juu ya tamko la pamoja.
Kwa upande mwingine viongozi wa ulimwengu wanaendelea kuhimiza mapatano kati ya Israeli na kundi la Hamas lakini kutokana na mashambulizi yanayoendelea idadi ya vifo katika mapigano hayo pia inaendelea kuongezeka.
Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric, watu zaidi ya 58,000 wamegeuka kuwa wakimbizi wa ndani kutokana na mashambulio ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza.
Ufaransa imesema bado inatafuta uwezekano wa kupatikana azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kusitishwa kwa mapigano hayo kati ya Israeli na kundi la Hamas la wapiganaji wa Kipalestina wanaoudhibiti Ukanda wa Gaza.
Unaweza kujiuliza kwa nini Umoja wa Ulaya hauna ushawishi kwenye mzozo unaoendelea katika eneo la mashariki ya kati?
Licha ya Umoja wa Ulaya kuwa mfadhili na muungaji mkono wa pande mbili za mgogoro mkongwe wa mashariki ya kati, ukweli ni kuwa si Jerusalem wala Gaza wanasubiri kauli za watu wa Ulaya kuutatuwa mzozo huo.
Kwa takribani miaka 25 sasa, Umoja wa Ulaya umekuwa ukiisaidia kifedha serikali ya Palestina, miradi ya maendeleo na elimu kwenye maeneo ya Ukanda wa Gaza, Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki.
Wenyewe Umoja huo unasema kwamba hutumia fedha nyingi zaidi kwa Wapalestina kuliko kwengine kokote katika eneo la Mashariki ya Kati.
Baina ya mwaka 2017 na 2020, mataifa ya Umoja wa Ulaya peke yao yalichangia jumla ya euro bilioni 2.3 kama msaada wa moja kwa moja kwa wananchi wa Palestina.
Kwa miaka mingi sasa, Umoja wa Ulaya umekuwa ukitoa msaada wa kijamii kwa zaidi ya watu 100,000 katika Ukanda wa Gaza, eneo linalotawaliwa na Hamas, ambalo kwa mujibu wa Umoja huo ni la kigaidi.
Umoja wa Ulaya pia unalipia sehemu ya mishahara na gharama za kiutawala za serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina yenye makao yake katika Ukingo wa Magharibi.
Haitoshi, kila mwaka euro milioni 159 hutolewa kwenye bajeti ya Umoja huo kwenda Shirika la la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina (UNWRA).
Kando ya fedha hizo, Ujerumani peke yake inachangia euro milioni 210 kwenye bajeti ya UNWRA.
Wakati huu ambapo Israel na kundi la Hamas wako kwenye mapigano, ilitazamiwa kwamba angalau Umoja wa Ulaya ungelikuwa na ushawishi wa kushinikiza usitishaji mapigano ambao unasema inataka kuuona na pia wenyewe kuwa sehemu muhimu ya upatanishi.
Lakini mchambuzi wa masuala ya Mashariki ya Kati katika Taasisi ya Sera za Ulaya mjini Brussels, Mihai Sebastian Chihaia, anasema ndani ya Umoja wa Ulaya kuna mpasuko linapohusika suala la Mashariki ya Kati.
Chihaia alisema katika umoja huo kuna mataifa yanayopendelea moja kwa moja Israel kama ilivyo Ujerumani na yanayoelemea Palestina kama ilivyo Sweden.
“Umoja wa Ulaya ina nyenzo zote muhimu za kuanzisha mkakati wa kusonga mbele kwenye eneo la Mashariki ya Kati. Lakini inahitaji dhamira ya kisiasa kuutekeleza mkakati huu. Dhamira hii ya kisiasa ndiyo ambayo imekosekana,” anasema Chihaia.
Kisiasa, Umoja wa Ulaya unaendelea kung’ang’ania suluhisho la madola mawili huru yanayoishi kwa usalama baina yao la Israel na la Palestina.
Lakini ili kulifikia suluhisho hilo, ambalo muda wote linazungumzwa bila kutekelezwa, kunahitajika usimamizi usioelemea upande wowote. Na huo, wachambuzi wengi wanaona, ni shida kupatikana ndani ya Umoja wa Ulaya.