KIGALI, RWANDA

RAIS wa Ufaransa Emmanuel Macron, amesema kuwa atafanya ziara nchini Rwanda mnami wiki ijayo ambapo ziara hiyo inachukuliwa kama mwanzo wa kuondosha mivutano ya muda mrefu na Rwanda.

Kwa muda wa miaka kadhaa, Rwanda na Ufaransa zinavutana kutokana na suala la mauaji ya kimbari yaliyotokea mwaka 1994.

“Ninathibitisha nitakwenda Rwanda mwishoni mwa mwezi huu. Hii itakuwa moja ya ziara ya kisiasa na kumbukumbu, lakini pia ya kiuchumi”, alisema Macron akiwa mjini Paris.

Aliongeza kuwa amekubaliana na rais wa Rwanda Paul Kagame, ambaye walikutana mjini Paris wiki iliyopita kwa ajili ya kuandika ukurasa mpya katika uhusiano baina ya nchi hizo.

Ziara yake itakuwa safari ya kwanza kufanywa na Rais wa Ufaransa tangu Nicolas Sarkozy alipoitembelea nchi hiyo mnamo mwaka 2010.

Kagame aliwaambia waandishi wa habari kutoka televisheni ya France 24 na Radio RFI Rwanda na Ufaransa zina msingi mzuri wa kuunda uhusiano baada ya ripoti ya kihistoria, iliyokiri Ufaransa ilikuwa na majukumu makubwa juu ya mauaji ya kimbari yam waka 1994.

Macron amejitahidi kurekebisha uhusiano na Rwanda kwa kuagiza ripoti ya kihistoria katika jukumu la wanajeshi wa Ufaransa kwenye mauaji ya kimbari, ambapo takribani watu laki nane waliuawa.

Ripoti hiyo ilihitimisha mwezi Machi kwamba Ufaransa ilikuwa gizani kwa maandalizi ya mauaji ya watu wengi wa kabila la Watutsi, yaliyofanywa na utawala wa wahutu, ambao waliungwa mkono na Ufaransa.

Katika siku za nyuma Kagame aliishutumu Ufaransa kwa kushiriki katika mauaji ya kimbari, lakini akasema alikubali matokeo ya tume ya Ufaransa kwamba Paris haikuhusika katika mauaji hayo.