NA KHAMISUU ABDALLAH

ALIYEDAIWA kujichukulia shilingi 5,000,000 kwa njia ya udanganyifu, kwa madai ya kuuza nyumba katika maeneo ya Mbuzini, amefikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.

Mshitakiwa huyo aliyetambulikana kwa jina la Iddi Mkubwa Nassor (48) mkaazi wa Kihinani wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Alifikishwa katika mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe, mbele ya Hakimu Fatma Omar na kusomewa shitaka linalomkabili na Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Soud Said.

Mshitakiwa huyo alidaiwa kuwa, Oktoba 6 mwaka jana majira ya saa 11:30 za jioni na Oktoba 8 majira ya saa 2:00 za asubuhi, huko Mwanakwerekwe wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja.

Alidaiwa kujipatia shilingi 5,000,000 kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa Rukia Abdulkadir Khamis, kwa kumuuzia kiwanja cha kujengea nyumba maeneo ya Mbuzini, huku akijua kuwa kiwanja hicho sio mali yake, hivyo hakumrejeshea fedha zake kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Wakili Soud alidai kuwa, kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu ni kinyume na kifungu cha 299 cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka hilo alikataa na kuiomba mahakama impatie dhamana, huku upande wa mashitaka ukidai kuwa upelelezi wake tayari umeshakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuwasilisha mashahidi.

Wakili Soud, akizungumzia suala la kupatiwa dhamana kwa mshitakiwa huyo alisema hana pingamizi ikiwa mshitakiwa huyo atawasilisha wadhamini madhubuti mahakamani hapo.

Hakimu Fatma, alikubaliana na ombi la upande wa mashitaka na kuiahirisha kesi hiyo hadi Juni 3 mwaka huu na kuamuru upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo, akiwemo mlalamikaji Rukia na mtoto wake Ali Haji Ali.

Hata hivyo, alimtaka mshitakiwa huyo kuwasilisha wadhamini wawili, ambao kila mmoja atamdhamini kwa shilingi 500,000 za maandishi na kuwasilisha vitambulisho vyao vya Mzanzibari mkaazi na barua za Sheha wa Shehia wanazoishi zinazoonesha nambari za nyumba.

Mshitakiwa huyo alikamilisha masharti hayo na yupo nje kwa dhamana hadi tarehe nyengine aliyopangiwa mahakamani hapo.