NA ASIA MWALIM

BARAZA la Manispaa Magharibi ‘B’ linatarajia kukusanya shilingi bilioni 200 kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Mkurugenzi baraza manispaa magharibi ‘B’, Ali Abdalla Natepe, aliyasema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya muelekeo wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kwa wajumbe wa baraza la madiwani la wilaya hiyo hafla iliyofanyika ukumbi wa baraza hilo.

Alisema fedha hizo zinatarajiwa kukusanywa kupitia vyanzo vyake vya ndani vya mapato ambapo kutasaidia kukuza uchumi na maendeleo ya wananchi.

Aidha alisema ongezeko hilo ni sawa na asilimia 2.3 ukilinganisha na bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 ambapok ulikusanywa bilioni mbili, milioni moja na 50.

Alifahamisha kuwa mwaka wa fedha 2021/2022 baraza la Manispaa Magharibi ‘B’ limejipangia kutekeleza malengo makuu manne ikiwemo kuongeza ukusanyaji wa mapato, kuimaririsha usafi wa mazingira, kukuza ustawi wa jamii na kupunguza umasikini kwa wananchi kwa kuwafikishia miradi na shughuli za maendeleo.

Mkurugenzi huyo alitaja lengo jengine ni kusimamia maslahi ya watendaji na madiwani wa baraza hilo ili kuimarisha shughuli za ofisi hiyo.

Mapema akitoa nasaha zake kwa wajumbe wa baraza hilo Mkuu wa Wilaya Magharibi ‘B’, Hamida Mussa Khamis, aliwataka madiwani kuisoma na kuelewa sheria inavyoelekeza katika utendaji ili kutekeleza ahadi walizotoa kwa wananchi katika wadi zao.

Alieleza kuwa sheria ya mamlaka za serikali za mitaa inaeleza na kuonesha wajibu wa mambo wanayopaswa kuyafanya watumishi wa baraza hilo ambapo kifungu cha 21 a hadi I, kimeeleza hayo.

“Sio kwa madiwani peke yao bali na watendaji waliomo ndani ya baraza wanapaswa kuijua sheria kwani walio wengi hawana uelewa juu ya sheria hiyo”, alisema Hamida.

Akichangia bajeti hiyo Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo ambae pia ni Diwani wa kuteuliwa Khalifa Ali Hamadi, alishauri uongozi wa baraza hilo kuongeza nguvu juu ya kutilia mkazo suala la ukusanywaji wa mapato.

Aidha alisema kuelekea bajeti 2021/2022 kamati inapendekeza uboreshwaji wa posho za madiwani na stahiki za wafanyakazi wa mikataba ikiwemo posho za muda wa ziada kwa wafanyakazi wote.