NA ALLY HASSAN, DOMECO
MKURUGENZI Msaidizi Baraza la Manispaa ya Mkoa wa Mijini Magharibi, Said Sudi Abdallah, ametowa wito kwa wananchi wa Mkoa huo na Wazanzibari, kuwa makini katika kipindi cha mvua za masika zinazoendelea kunyesha, ili kuepuka maafa yakiwemo maradhi ya mripukpo.
Akizungumza na Zanzibar Leo ofisini kwake, Saidi alisema wakati mvua zinaendelea kunyesha katika maeneo mbali mbali ya visiwa kuna maafa mengi hujitokeza yakiwemo nyumba kujaa maji, maradhi ya mripuko sambamba na nyuba kuangukiwa na miti.
Alisema kuna baadhi ya watu wana tabia ya kutupa magunia ya taka na mipira ya gari kwenye mitaro ya kupitishia maji na kusababisha mitaro hio kuziba na kupelekea maji taka kutuama katika makaazi ya watu.
“Nawaombeni ndugu zangu wa Manispaa yetu ya mjini tuwe makini na watu wenye tabia ya kuchafua mazingira kwa sababu tukimruhusu mtu kutia polo la taka katika michirizi ya maji, itakapoziba waathirika wa kwanza ni nyie munao kaa hapo,”alisema.
Said alisema kila mtu aweze kutunza sehemu yake inayo mzunguka na kama itatokezea mtu amekwenda kinyume nao wasisite kutoa taarifa katika Manispaa ya Mjini, ili aweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Aidhaa, Mkurugenzi Msaidizi huyo aliwataka wale walio jenga karibu na miti mikubwa kuchukua tahadhari kama kutakuwa na dalili yoyote ambayo ita hatarisha usalama wao na nyumba zao watoe taarifa mapema manispaa, ili watoe ushirikiano wa kupunguzwa matawi ya miti hio.
“Hakika Baraza la Manispaa ya Mjini linakupendeni wananchi wetu hasa Serikali yetu hii ya awamu ya nane ni serikali sikivu chini ya Rais wetu kipenzi Dr. Hussein Ally Mwinyi, tuko wasikivu sana na tuko tayari kuwafatilieni na kuwasaidieni kuwatatulia shida zenu wananchi,” alisema.
Saidi amewataka wananchi walio jenga karibu na maeneo yanayo tuama maji kipindi cha mvua kubwa zinapo nyesha kuchukue hatua za mara moja kuhama maeneo hayo, ili kuepukana maafa yatakayo jitokeza.