Kuwa maeneo ya uwekezaji viwanda
NA KHAMISUU ABDALLAH
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema serikali imechukua uamuzi wa kuyageuza mashamba ya mpira kuwa eneo jipya la viwanda ili kutoa fursa ya ajira kwa vijana.
Dk. Mwinyi alitoa kauli hiyo wakati akitembelea mashamba ya mpira Selemu, kiwanda cha Mpira mkiwa na shamba kichwele Mkoa wa Kaskazi Unguja.
Alisema, hatua hiyo imekuja baada ya kupewa taarifa serikalini kwamba yapo mashamba ya mpira ambayo hayatumiki kama inayotarajiwa na tija yake ni ndogo.
Aidha alisema serikalini baada ya kutafakari jambo hilo wameona kuwa mashamba ya mpira hayana tija na wala hayamsaidii mtu yoyote sio kwa ajira wala kipato cha serikali.
Dk. Mwinyi alisema mtaalamu anasema mpira una kiwango cha miaka 30 katika uzalishaji na baadae kushuka na kutozalisha tena kwa tija.
Hata hivyo alisema sababu nyengine ya serikali kutoa uamuzi huo kunatokana na muwekezaji aliyopewa kazi hiyo ameshindwa kulipa fedha anazodaiwa na serikali, madeni aliyokopa benki na kushindwa kuwalipa wafanyakazi wake stahiki walizokuwa wanadai.
Alisema waliahidi kuwa nchi itahitaji kuwa na viwanda vingi ili watu waweze kupata ajira
“Kama una hekta 1270 ambazo hazizalishi na hakuna anaepata basi tumeona kuwa ni busara maeneo haya yakatumika kwa kutafuta wawekezaji ili waweze kutengeneza viwanda ambao tayari wameshajitokeza kuwa na nia hiyo, wanachotaka ni kupewa ardhi tu ambayo itakuwa na huduma ya maji na umeme waanze kazi,” alibainisha.
Mbali na hayo alibainisha kuwa lengo la serikali kumkabidhi muwekezaji hekta 623 itaweza kukidhi haja.
Aliahidi kuwa matatizo aliyoyaacha muwekezaji yanashughulikiwa kabla ya kuanza mipango mipya ili kuanza ukusara mpya na kuwatoa hofu wafanyakazi katika mashamba hayo.
Hata hivyo alibainisha kuwa serikali inataka kufanya mambo mazuri kwa nchi na litakaloingiza kipato katika mashamba hayo.
“Badala ya kukaa na mali kubwa kama hii ambalo ni pori tu hakuna anaefaidika sasa wakati umefika maeneo haya yatengenezwe ili yawe yanatija kwa serikali na wananchi wake.
Mbali na hayo, alipongeza wizara ya kilimo kwa kupeleka taarifa kamili ya mashamba hayo ili kuiwezesha serikali kufanya maamuzi mazuri kwa mustakabali wa taifa.
Hata hivyo Dk. Mwinyi aliwaomba viongozi wa mikoa husika yenye mashamba hayo kuliunga mkono jambo hilo ambalo litaweza kutoa ajira kwa vijana wazawa wa maeneo hayo.
Alisema Chama cha Mapinduzi kiliahidi katika ilani yake kuwa itatengeneza ajira 300,000 katika miaka mitano ya utawala wa serikali ya awamu ya nane hivyo ni lazima kuanza hasa katika sekta ya viwanda ukiacha sekta ya uchumi wa bluu.
Mbali na hayo alisema Zanzibar hakuna kitu kinachozalishwa na badala yake vitu vyote vinaagizwa kutoka nje ya nchi hivyo hivi sasa hakuna sababu ya vitu nyengine kutoka nje na badala yake kuzalisha hapa hapa nchini kupitia viwanda hivyo.
Wakati huo huo Dk. Mwinyi akitembelea shamba la serikali Msumbiji aliiagiza wizara ardhi kuhakikisha inaweka utambulisho ‘bacons’ ili kuweka usalama wa mashamba yake kutovamiwa.
Kwa upande wa wizara ya kilimo, Dk. Mwinyi alisema ni lazima utoaji wa mashamba kwa wawekezaji ufanywe na Mamlaka ya Ukuzaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) kwa maeneo yote ili kuondoa usumbufu kwa wawekezaji na kuondoa urasimu katika jambo hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud aliahidi kuendelea kutekeleza agizo la kuwaelezea wananchi kwa vitendo juu ya dhamira njema ya serikali katika mashamba hayo.
Alisema wakipata hekta 760 katika uwekezaji wa viwanda na ukifanyika vizuri wananchi wa mkoa wa Kasakazini Unguja, wazanzibari na Tanzania kwa ujumla wataweza kupata fursa kubwa ya ajira na kipato.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Maliasili na Mifugo, Dk. Maryam Juma Sadala, alisema mashamba ya Mipira yote kwa Unguja na Pemba yana hekta 1,270 ambapo kwa Unguja ni hekta 633 na Pemba ni hekta 637
Alisema upandaji wa mipira hiyo ulianza katika miaka ya 78 hadi 82 kwa lengo la kuongeza pato la taifa na kuwapatia ajira wananchi.
Aidha, alisema uzalishaji wa mpira ulianza kushuka kwani mwaka 2015 kulizalishwa tani milioni 4,229 lakini mwaka 2014 tani 400.
Hata hivyo alibainisha kuwa sababu nyengine ni ugemaji wa mashamba hayo uliosababisha mpira kupata maradhi ikiwemo kenka na uvamizi wa mashamba.