WAZIRI wa Afya Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui, amesema kutokana na miundombinu na udogo wa viwanja vya ndege na bandari mashine maalum za kupimia joto kwa wasafiri zimekuwa zikiharibika mara kwa mara.
Akijibu suala la msingi liloulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Nafasi za Wanawake, Fatma Ramadhan Mandoba, katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, alietaka kujua kwa nini mashine hazitumiki kwa lengo lilokusudiwa la kuwapima joto la mwili wasafiri wanaoingia katika bandari na viwanja vya ndege.
Alisema kwa mujibu wa taarifa za kitaalamu kutoka kwa mafundi wa mashine hizo kuharibika mara kwa mara kutokana na ukaribu wa eneo zilizopo mashine hizo na eneo la nje ya uwanja, na mashine huchukua joto la nje ya uwanja na kusababisha kupanda sana kwa vipimo joto husika.
Alisema kutokana na hali hiyo hulazimika kutumia vipima joto vya mikononi ili kufikia lengo lilokusudiwa.
Aidha alisema, serikali kupitia Mamlaka ya viwanja vya ndege na Wizara ya Afya, inaendelea kuzifanyia marekebisho mashine maalum za kupimia joto, ili ziendane na hali ya viwanja huku ikiendelea kutumia vipima joto vya mkononi.
Hata Hivyo, alisema tayari Wizara imeshapeleka mashine mbili mpya za aina hiyo, zinazotegemewa kufungwa katika uwanja mpya wa ndege wa Abeid Amani Karume Taminal 111 mara tu baada ya kuanza kazi.
Alisema anaamini kuwa kutokana na ukubwa wa Uwanja huo mashine hizo hazitoweza kuharibika mara kwa mara.
Akijibu suala la Shadya Mohammed Suleiman, alietaka kujua serikali ina mpango gani wa kuweka mashine hizo katika kiwanda cha ndege Pemba, alisema serikali inampango wa kutafuta mashine hizo kwa kiwanja hicho lakini kukipatikana eneo kubwa la kuziweka.