NA RAJAB MKASABA, IKULU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza Umoja wa Mataifa (UN), kwa azma yake ya kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kukuza uchumi na kuimarisha ustawi wa jamii.
Dk. Mwinyi alitoa pongezi hizo jana wakati alipofanya mazungumzo na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN), nchini Tanzania, Zlatan Milisic ambaye alifika ikulu Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha rasmi kwa Rais.
Rais aliupongeza Umoja wa Mataifa kupitia mashirika yake kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na kutoa mashirikiano katika kuendeleza miradi kadhaa ya maendeleo ambayo ina tija kwa ustawi wa wananchi.
Dk. Mwinyi alimueleza Mratibu huyo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na juhudi za kuimarisha uchumi kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi ikiwa imeweka kipaumbele katika utekelezaji wa mipango na sera za Uchumi wa buluu.
Katika mazungumzo yake hayo alieleza kuwa hali ya amani na utulivu ya Zanzibar imezidi kuimarika kutokana na mashirikiano mazuri yaliyopo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambapo kipaumbele ni kuhakikisha kunaimarishwa maendeleo.
Aliongeza kwamba kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kumeipelekea Zanzibar kuimarika kisiasa, kiuchumi na kijamii na kueleza matumaini yake ya kupata maendeleo zaidi kutokana na mashirikiano hayo yaliyopo.
Alieleza kwamba kuibuka kwa maradhi ya COVID 19 duniani kumesababisha sekta ya utalii kuzorota, sekta ambayo inategemewa kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha pato la Taifa na uchumi wa Zanzibar.
Dk. Mwinyi alieleza haja kwa Umoja huo kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya hasa katika kuimarisha miundombinu na mifumo ya utoaji huduma na uendeshaji.
Alifahamisha haja ya kuendelea kuungwa mkono katika kupambana na vifo vya akina mama na watoto na kusema kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa la UNICEF, ambalo limekuwa mdau mkubwa wa Zanzibar katika kuisaidia kuendeleza sekta ya afya lakini hata hivyo, juhudi za makusudi zinahitajika ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Aidha, alieleza haja kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) la kuhakikisha linauenzi Mji Mkongwe wa Zanzibar ambao ni Urithi wa Dunia, kwani hivi sasa baadhi ya nyumba nyingi katika mji huo kuhitaji matengenezo kutokana na uchakavu wake.
Alieleza kwa upande wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Afya Ulimwenguni, Dk. Mwinyi alieleza haja kwa Shirika hilo kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya hasa katika kupambana na maradhi ya COVID 19.
Dk. Mwinyi alisema kuwa hivi sasa Zanzibar inaandaa utaratibu wa kuwawezesha mahujaji kupata tiba ya chanjo ya COVID 19 ili kukidhi vigezo vilivyowekwa na Serikali ya Saudi Arabia mwaka huu katika kushiriki ibada hiyo tukufu hatua ambayo mashirika ya Umoja huo yanaweza kuiunga mkono Zanzibar ili kufikia matakwa hayo.
Naye Mratibu Mkaazi wa Umoja wa Mataifa (UN), nchini Tanzania Zlatan Milisic alimueleza Dk. Mwinyi azma ya Umoja huo ya kuisaida Zanzibar katika kuendeleza miradi ya maendeleo na kuhakikisha mashirika yote yaliyopo Tanzania.
Zlatan Milisic alitumia fursa hiyo kumpongeza Dk. Mwinyi kwa kuchaguliwa na wananchi wa Zanzibar kwa kishindo katika uchaguzi mkuu uliopita huku akieleza azma ya UN ya kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha miradi inayosimamiwa na mashirika yake inaleta manufaa kwa wananchi wa Zanzibar.
Alipongeza mashirikiano na uhusiano mzuri uliopo kati ya mashirika ya UN na Zanzibar na kueleza kwamba Umoja huo utaongeza nguvu katika kuhakikisha mafanikio zaidi yanapatikana hasa katika uchumi wa Zanzibar ukiwemo uchumi wa buluu.