LONDON, UINGEREZA
UPIGAJI kura katika uchaguzi wa Bunge la Scotland umemalizika lakini sasa inapaswa kusubiri kuhesabu kura kuanza.
Kura zilianza kuhesabiwa usiku wa manane hapo juzi ambapo baadae zoezi hilo liliakhirishwa kwa sababu ya vizuizi vya Covid na zoezi hilo kuendelea jana Ijumaa huku matokeo yakitarajiwa kutolewa leo Jumamosi.
Idadi kubwa ya watu tayari walikuwa wamepiga kura zao kabla ya kura kufunguliwa – na zaidi ya milioni moja walikuwa wamejiandikisha kupiga kura kwa njia ya posta.
Uchaguzi huo unaonekana kuwa muhimu kwa mustakabali wa Uingereza kwani matokeo yanaweza kuathiri ikiwa kuna kura ya maoni ya pili juu ya uhuru wa Scotland.
Uchaguzi wa Scotland, sehemu ya Uingereza yenye mamlaka ya ndani ndio unaangaziwa kwa makini, kwa sababu chama kinachotawala jimbo hilo SNP kinataka kura mpya ya maoni kuhusu uhuru wa Scotland.
Uchaguzi huu pia unachukuliwa kama kipimo cha uungwaji mkono wa chama cha Conservative cha Waziri Mkuu Boris Johnson, juu ya namna kinavyoiongoza nchi baada ya kukamilisha mchakato wa Brexit na namna utawala wake unavyolishughulikia janga la COVID-19.
Katika ujumbe wake kwa wapigakura kupitia mtandao wa twitter, Johnson aliwataka kujitokeza kwa wingi na kukiunga mkono chama chake, akisema ndicho kinachoyajali maslahi yao, na kudai kuwa hoja za vyama vingine ni porojo tu za kisiasa.