NAIROBI, KENYA

MBUNGE wa Gatundu Kusini nchini Kenya, Moses Kuria ameibua shutuma mpya dhidi ya wabunge wa nchi hiyo, baada ya kudai kwamba kuna baadhi ya wabunge wa bunge la taifa wamehongwa ili wapitishe mswada wa maridhiano (BBI).

Mbunge huyo alidai kuwa kiongozi wa wengi bungeni Amos Kimunya, ana husishwa kuwahonga wabunge ili kupigia kura ya kuunga mkono michakato inayofadhiliwa na serikali.

Mwanasiasa huyo wa Gatundu Kusini alisisitiza madai kwamba wabunge walipokea shilingi 100,000 za nchi hiyo kila mmoja ili kupitisha mswada wa BBI.

Jumla ya wabunge 224 wiki iliyopita walipiga kura ya kuunga mkono mswada huo dhidi ya 63 ambao walikataa, ambapo mbunge huyo Gatundu alisema mswaada huo umepigiwa kura kwa rushwa.

“Kimunya … unafikiri wewe ni nani? Ikiwa waheshimiwa wanachama wataamua kuptishwa mswaada kwa sababu ya shilingi 100,000 pekee hilo linanihusu na nini? Nimekula shilingi 100,000 yako mara nyingi mno, lakini sitawahi kuisaliti dhamira yangu”, alisema.

“Wabunge wanapiga kura ya ndiyo kwa sasa wanapokea KSh 100,000 zao kutoka kwa afisi ya kiongozi mkuu katika bunge,” Kuria alichapisha kwenye Facebook.

Jumla ya wabunge 247 walikuwepo ndani ya Bunge, wakati wengine 55 ambao hawakujitokeza kwalijsajili kushiriki zoezi la kupiga kura kwenye mtandao.

Mbunge wa Kitui ya Kati Makali Mulu alizungumzia suala hilo, akisema Moses Kuria aliwapaka matope wabunge wenziwe kwa kutoa madai hayo.

“Haya ni makosa sana kutoka kwa kiongozi anayeheshimika, wakati mwingine mambo katika bunge hufanywa kwa njia ya kawaida”, alisema.

Wabunge wengine waliwataja wenzao kama wanaoweza kununuliwa, waoga na wasaliti,” Mulu alisema.

Spika Justin Muturi aliwaambia wabunge kwamba amewaagiza Kuria, wabunge Ndindi Nyoro na Mohammed Ali kufika mbele ya kamati ya Bunge kutoa ushahidi wa tuhuma zao.