NA MADINA ISSA

MBUNGE wa Jimbo la Kikwajuni, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni,  ameahidi kushirikiana na serikali katika kusaidia mahitaji mbali mbali ya kambi za wanafunzi wa skuli zilizopo ndani ya jimbo hilo, ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi na kuinua sekta ya elimu nchini.

Ahadi hiyo, alitoa katika ghafla ya kuwakabidhi bidhaa za vyakula kwa ajili ya kambi ya  wanafunzi wa  skuli ya Dk. Ali Mohamed Shein iliyopo Mwembeshauri Mkoa wa Mjini Magharib ambapo jana wanafunzi wake walianza kufanya mtihani.

Alisema hatua hiyo ni muendelezo wa juhudi atazozifanya katika jimbo hilo, ikiwa ni moja ya mikakati ya kuimrisha sekta ya elimu kwa kuongeza ufaulu wa wanafunzi.

Aidha alisema kuwa kuwepo kwa utaratibu huo, utaweza kuwasaidia wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kuengezeka ufaulu huo, pamoja na kuwapongeza walimu kwa jitihada zao wanazozifanya katika skuli zilizopo katika jimbo hilo.

Hata hivyo, alisema kuwa hakuna sababu yaoyote ya skuli iliyopo katika jimbo hilo kushindwa kuweka kambi kwa ajili ya maandalizi ya mitihani kwa kutokuwa na uwezo wa vyakula pamoja na vitendea kazi .

Alisema ndani jimbo hilo kuna mfuko wa jimbo unaowasaidia sana katika kuona elimu ya skuli na dini inakuwa na kuweza kufaulu vizuri.

Mwalimu wa skuli hiyo, Seif Adam Muhunzi, alisema juhudi hizo zinazofanywa na Mbunge na viongozi wengine wa jimbo zinafaa kuwa endelevu sambamba na kuangalia namna ya kutatua changamoto nyengine zinazojitokeza katika sekta hiyo.