NA MWANDISHI WETU

SIMBA inaweza kutwaa ubingwa  ndani ya mechi sita zijazo za ligi kuu Tanzania Bara.

Simba inaongoza msimamo na pointi 61 ina mechi 11 mkononi, kama itashinda sita mfululuzo, itafikisha pointi 79.

Pointi hizo haziwezi kufikiwa na timu nyingine ikiwamo Yanga ambayo ikishinda mechi zake zote itafikisha pointi 76. Mechi hizo sita za Simba ni dhidi ya Namungo, Ruvu Shooting, Polisi Tanzania, Mbeya City, Yanga na KMC.

Baada ya hapo itakuwa imebakisha mechi dhidi ya Coastal Union, Azam na Namungo kumaliza msimu ambazo hizo zitakuwa za kulinda heshima.

Yanga tayari imesisitiza kuwa inacheza ligi kutafuta matokeo na habari ya nani atakuwa bingwa itajulikana kwenye mchezo wa mwisho ambapo Yanga itakuwa ugenini dhidi ya Dodoma Jiji na Simba itacheza nyumbani na Namungo.

Baada ya Bodi ya ligi kuipanga upya mechi ya Simba na Yanga ipigwe Julai 3, Simba wamewambia Yanga  wapange muda kabisa kuondoka mkanganyiko.

Awali, mechi hiyo ilikuwa ipigwe Mei 8 lakini iliahirishwa baada ya Yanga iliyokuwa kwenye nafasi ya pili kwenye msimamo na pointi 57 kuondoa timu uwanjani ikipinga mabadiliko ya muda wa mchezo kutolewa ndani ya muda mfupi.

“Niwakumbushe tu watani kwamba tunaweza kucheza mechi hiyo tukiwa mabingwa, hivyo kama itawabidi kujipanga kumpa heshima bingwa, basi wasisite.”

Kuhusu ratiba mpya ya kucheza Julai 3, Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema; “Tumeipokea, hivyo tusubiri muda ufike.”