NA ZAINAB ATUPAE
UONGOZI wa soka Mkoa wa Mjini Magharibi umesema msimu huu umejipanga kutoa zawadi nzuri kwa washindi msimu huu.
Akizungumza katika kikao na viongozi wa timu zinazoshiriki ligi ya Mkoa huo katibu wa chama hicho Ahmada Haji Khamis,alisema lengo la kufanya hivyo ni kuleta ushindani kwa timu hizo na kuimarisha ligi yao ili kuwa mfano kwa ligi nyengine.
Alisema wanatarajia kutoa zawadi kwa mshindi wa kwanza ambae atapata nafasi ya kupanda daraja kutoka Mkoa na kwenda la Kwanza kanda mshindi wa pili na mshindi wa tatu.
Alisema mbali na hapo wanatarajia kutoa zawadi kwa mshindi wa nne endapo hali ikiruhusu.
“Tuna mpango mkubwa wa kutoa zawadi kwa mshindi wa nne tunaendelea kutafuta tukifanikiwa na wao watapatiwa zawadi zao,”alisema Ahmada.
Alisema zawadi nyengine zitakwenda kwa timu itakayokuwa na nidhamu,mwamuzi bora, mchezaji bora,kipa bora na kiongozi atakae kuwa na nidhamu.
Alisema zawadi wanazotarajia kutoa ni pamoja na pesa taslimu,makombe,mipira pamoja na jezi.
Aidha aliwataka viongozi wa timu kuacha kufanya makosa ya sio na msingi,ili kupunguza adhabu ambazo hazina msingi.
Hivyo aliwataka viongozi wote wanao daiwa kumaliza madeni yao kabla ya kuanza kwa mzunguruko wa pili.