NA KHAMISUU ABDALLAH

MKUTANO wa tatu wa Baraza la 10 la Wawakilishi utakaojadili bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022 unatarajiwa kuanza rasmi Mei 5 mwaka huu.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa Baraza la Wawakilishi Raya Issa Mselem wakati akitoa taarifa kwa vyomb vya habari katika ukumbi wa Baraza hilo Chukwani.

Alisema katika mkutano huo pia kutakuwa na shughuli mbalimbali ikiwemo kiapo cha mjumbe wa Baraza la Wawakilishi jimbo la Pandani alieshinda katika uchaguzi mdogo uliofanyika Machi 28 mwaka huu kufuatia kifo cha aliyekuwa Mwakilishi mteule wa Jimbo hilo Abubakar Khamis Bakar, kufariki dunia Novemba 11 mwaka 2020.

Aidha alisema jumla ya masuali ya msingi 218 yataulizwa na kujibiwa katika mkutano huo.

Raya alisema miswaada miwili ya sheria itawasilishwa na kujadiliwa katika mkutano huo ikiwemo mswada wa sheria ya fedha (Finance Bill) na mswada wa sheria ya kuidhinisha matumizi ya serikali kwa mwaka 2021/2022.

Hata hivyo, alibainisha kuwa mbali na shughuli hizo pia wanatarajia kuwa na miswada ya sheria itakayosomwa kwa mara ya kwanza barazani hapo kutoka serikalini.

“Wakati wowote kuanzia sasa tunaweza kupokea miswada hii ambayo itasomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano huu lakini jambo lolote litakaloweza kujitokeza linaweza kufanyiwa kazi na Spika,” alibainisha.

Katibu Raya, aliwaomba wananchi kushirikiana na baraza hilo na wajumbe wake ambao ni wawakilishi wao waliowatuma katika chombo hicho ili kuwawakilisha.

“Tunawaomba wananchi wawape ushirikiano wawakilishi wao waliowachagua kwani ushirikiano wao ndio utakaoweza kufanikisha shughuli yetu ya mkutano huu wa tatu,” alisisitiza.

Katika hatua nyengine, Raya alivipongeza vyombo vya habari vya Zanzibar, Tanzania bara na dunia nzima kwa ujumla katika kuadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari inayoadhimishwa kila ifikapo Mei 3 ya kila mwaka duniani kote.

Aliwaomba wanahabari kushirikiana na baraza na serikali kwa ujumla katika kupeleka habari kwa wananchi ili kujua mambo mbalimbali yanayofanywa na serikali kwa wananchi wake.

Aliahidi kushirikiana na vyombo vyote vya habari vilivyokuwepo nchini ambao ni wadau wakuu katika kupeleka gurudu la taifa la Tanzania katika maendeleo.