KIGALI, RWANDA
MWANAMKE aliyefukuzwa Marekani na kurejeshwa nchini Rwanda, amekanusha mashitaka ya makosa ya mauaji ya kimbari ya mwaka ya mwaka 1994, akisema wakati huo anaodaiwa kuhusika na mauaji hayo alikuwa mjamzito.
Béatrice Munyenyezi, hivi karibuni alirejeshwa kutoka Marekani alikokuwa amejificha kukwepa mkono wa sheria kutokana na kuhusishwa na mauaji ya kimbari.
Hata hivyo alisema, wakati mauaji hayo yanatokea alikuwa mjamzito. “Kuwa na mapacha na kuwa mjamzito, ningewezaje kushiriki kwenye mauaji ninayodaiwa kutekeleza?” ameiambia mahakama.
Munyenyezi anakabiliwa na mashitaka saba ya mauaji yenye kuhusishwa na uhalifu kuanzia mauaji hadi ubakaji.
Kulingana na ushahidi uliotolewa wakati wa kusikiliza kwa kesi ya mume wake na mama mkwe wake katika mahakama ya Umoja wa Mataifa huko Arusha, Tanzania, Munyenyezi alishutumiwa kwa kusimama katika vituo vya ukaguzi barabarani kubaini watu wa jamii ya kitutsi ili wauawe.
Aidha anatuhumiwa kuhusika kuwahamasisha wanamgabo wa kihutu kubaka wanawake kabla ya kuwaua huko Butare, mji wa kusini mwa Rwanda.
Akishtumiwa kwa kuwa mwenye ushawishi katika mauaji ya wanafunzi wa kitutsi mjini humo, Munyenyezi amekanusha madai hayo akisema alikuwa mgeni na hakuwa ameenda kwenye vituo vya ukaguzi barabarani.
Alisema aliwasili Butare Julai 1993 na kuolewa akiwa na ujauzito wa miezi miwili, akajifungua mapacha na muda mfupi baada ya hapo akapata tena ujauzito mwingine.