KIGALI, RWANDA

MAHAKAMA ya Rwanda imemhukumu mwandishi wa habari Phocas Ndayizera na wengine sita kfungo cha miaka 10 gerezani kwa mashtaka ya ugaidi.

Wamekutwa na hatia kwa kosa la kupanga kulipua eneo la umma katika mji mkuu wa Kigali na kula njama za kufanya ugaidi.

Jaji alisema mahakama ingeweza kuwapa kifungo cha miaka 20 na 25 “lakini wamepewa miaka 10 kwasababu mpango wao haukufanikiwa na hivyo haukusababisha athari kwa umma”.

Katika mkutano wa kwenye video uliofanyika Alhamisi mchana, wengine sita mahakama iliamuru waachiwe huru kwa mashtaka yanayowakabili.

Mwezi Novemba 2018, mwandishi Phocas Ndayizera alipotea kwa siku saba kabla ya kufikishwa polisi wiki moja baadae wakati walipokamatwa kwa makosa ya kufanya mpango wa shambulio la mlipuko. Ndayizera na wenzake wamekanusha mashtaka hayo yote.