NA ZAINAB ATUPAE

KATIBU wa timu ya mpira wa miguu ya Mwera City Fahad Ali Kai,amewataka wachezaji wa timu hiyo kufika mazoezini baada ya kumalizika sikukuu kujiandaa na mechi zilizo bakia.

Mwera City inashiriki ligi daraja la pili wilaya ya Magharibi’A’ Unguja inashika nafasi ya kwanza katika kundi ‘A’ikiwa na pointi 11 kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Akizungumza na  gazeti hili katibu huyo alisema wanatarajia kuanza mazoezi mapema, kwani malengo yao ni kuchukua ubingwa na kuipandisha daraja msimu huu.

Alisema kutoka na malengo hayo aliwataka wachezaji kutambua kuwa baada ya kumalizika sikukuu watatakiwa kurudi uwanjani kuendelea na mazoezi na kusubiria ratiba ya kumalizia mzunguruko wa pili.

Aidha alisema kabla ya kuanza kwa mazoezi wanatarajia kukutana na viongozi na makocha wa timu kujadili baadhi ya changamoto zilizojitokeza katika mechi zote walizocheza kwenye mzunguruko wa kwanza.

“Kabla ya kuanza mazoezi takutana na viongozi na makocha kujadili mambo mbali mbali hasa yaliojitokeza katika mechi tulizocheza na kuyafanyia marekebisho ili yasijekujitokeza katika mechi zilizobakia,”alisema.