Usafiri, baadhi ya vituo vya polisi kutofanya kazi, kubadilisha taarifa za walalamikaji

NA MWAJUMA JUMA

KATIKA kufikia ndoto ya kweli ya kumaliza unyanyasaji na ukatili wa kijinsia Zanzibar kuna changamoto nyingi zinazokwaza mukhtadha wa tatizo hilo.

Mbali na muhali, rushwa, ushirikiana, kutotoa ushahidi, kukubaliana kwa wanajamii na familia lakini jambo jengine lililobainika ni changamoto ya usafiri kwa jeshi la polisi kuwafuatia watuhumiwa.

Makala haya imeonesha kwa kina namna tatizo hilo kwa baadhi ya vituo vya polisi jambo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi ili isiwe kizingitoi cha kufikia dhamira ya dhati.

Hivyo, makala haya ilizungumza na vyanzo mbalimbali ili kuona ni hatua gani itachukuliwa kukabiliana na hali hiyo.

Matatizo ya usafiri katika madawati ya Jinsia, wanawake na watoto ya

Jeshi la Polisi limeeelezewa kwa muda mrefu kuwa kikwazo katika

kufuatilia kesi za udhalilishaji wa kijinsia.

Hali hii imesababisha polisi kulalamikiwa namna inavyopambana na vitendo

Hivyo hasa katika kuwafuatilia na kuwashughulikia kisheria watu wanaodaiwa

kufanya vitendo vya udhalilishaji hapa Zanzibar.

Malalamiko haya yalepelekea Chama Cha Waandishi wa Habari wanawake

Tanzania (TAMWA Zanzibar) kuandaa dodoso maalumu la kutaka kujua kwa

kiasi gani limefanyiwa kazi ili kundoa malalamiko hayo na kuhakikisha

wanaofanya vitendo hivyo wanawajbishwa kisheria.

Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai  katika Makao Makuu ya Polisi Ziwani, Hamad Khamis Hamad, alisema wameshaanza kulifanyiia kazi tatizo hilo na wanatarajia kulimaliza kadri hali ya kifedha itaporuhusu.

Hata hivyo, alisema usafiri sio tatizo pekee katika jeshi hilo katika

Vituo, bali hata katika makao makuu zipo changamoto ambazo wanaendelea

kufanya juhudi za kupata ufumbuzi.

Alieleza kwamba Jeshi la Polisi hupanga shughuli zake kwa kutegemeana na

bajeti iliyoidhinishwa na Serikali na yapo matatizo mengi ukitilia maanani ukubwa wa taasisi hii.

Hata hivyo aliwashukuru wadau mbali mbali kwa msaada wao na kuomba ushirikiano huo uendelee ili ufanisi katika Jeshi la Polisi uwe mzuri zaidi.

“Kwa mfano, vituo vingi vya Polisi vipo katika hali mbaya na vipo

ambavyo ujenzi wake umesimama kutokana na uhaba wa fedha, miongoni

mwao kikiwa kituo cha Uwanja wa Ndege wa Zanzibar”, alisema.

KUBADILISHA MAELEZO

 Jambo jengine lililobainika katika utafiti mdogo ni pamoja na Polisi ikudaiwa kuhusika na kubadilisha maelezo ya mlalamikaji katika baadhi ya kesi za udhalilishaji, lakini Hamad anasema hilo halina ukweli kwa maelezo ya kwamba mlalamikaji  hutakiwa kusoma maelezo yake na kama hajui kusoma husomewa neno kwa neno na baadae ndio huweka saini yake.

“Saini hio huwekwa katika kila karatasi ya maelezo ili kuepuka kubandika

karatasi ya maelezo ya kughushi baada ya kuchomolewa karatasi ya maelezo halisi yaliyotolewa”, alisema.

UFUATILIAJI MAAFISA WANAOHARIBU KESI

 Naibu Mkurugenzi huyo wa makosa ya Jinai, alisema kuwa hivi sasa Jeshi la Polisi limeweka  muongozo maalumu  wa kubaini maafisa na askari wanaolalamikiwa kuharibu kesi na tayari wapo askari waliowajibishwa kwa makosa mbali mbali, yakiwemo ya udhalilishaji wa kijinsia.

Alisema kati ya makosa hayo, wapo waliofukuzwa kazi, kusimamishwa au kupewa onyo na kushushwa vyeo.

“Hatua hii inakwenda sambamba na utoaji wa elimu ya masuala ya

udalilishaji kwa jamii kwa kupitia sehemu mbali mbali, ikiwemo maskuli na vyombo vya habari.

MWAMKO WA KURIPOTI KESI ZA UDHALILISHAJI

 Hivi sasa vitendo vya udhalilishaji ni suala mtambuka ambalo linagusa

mtu mmoja, familia, jamii na nchi kwa ujumla na kwa hivyo kila mtu

anayo nafasi yake ya kupambana navyo.

Hamad alisema jambo muhimu ni kwa kila mtu kuangalia mwenendo wa mtoto wake na wa mwenzake na kuangalia malezi ya watoto yakoje kutokana na kuwepo

baadhi ya familia kuwaachia watoto kufanya wanavyotaka na kupelekea

kuwepo ugomvi wa kila siku ndani ya familia.

Aidha utafiti unaonyesha kuwepo kwa udhalilishaji kunachangiwa na umasikini

ambao unapelekea mtoto bila ya yeye mwenyewe kujua kukata tamaa ya maisha.

Hamad alisema utoaji wa taarifa za udhalilishaji kwa jeshi la polisi kwa

sasa bado ni changamoto kwa sababu mbali mbali, kama wengine kuhisi

kutoa taarifa ni kuzidi kujidhalilisha.

“Kwa mfano suala la kubaka au kulawitiwa hutegemea mtu anavyolipokea

wengine huona aibu kwenda kituo cha polisi kusema amebakwa au

kalawitiwa, kwa hivyo anaona bora akae kimya”, alisema.

Wengine huona ni vizuri pakishatokea udhalilishaji badala ya kuripoti

Polisi familia mbili zilizohusika huona bora zikae na kumalizana, lakini hilo sio suluhisho muwafaka.

Kama zilivyo taasisi nyingi na jamii, Jeshi la Polisi limeupokea kwa

furaha uamuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) wa kuanzisha

mahakama maalumu ya kesi za udhalilishaji wa kijinsia na Polisi

wanaamini hatua hii itashajiisha jamii kuripoti matukio ya

udhalilishaji badala ya kuyamaliza kimya kimya.

“Tayari Polisi imeshuhudia mabadiliko kwa kujitokeza watu wengi kutoa

taarifa za matukio haya, tafauti na hali ilivyokuwa hapo kabla”, alisema.

Hamad alisema kuongezeka kwa taarifa hizo hakumaaanishi kuzidi kwa

matokeo bali inatokana na jamii kuanza kuvunja ukimya na kutaka sheria

ichukuwe mkondo wake badala ya kuwasamehe kienyeji wanaofanya uovu huo.

Tokea kuanzishwa kwa mahakama maalum ya udhalilishaji jumla ya kesi 278 zimefunguliwa na Polisi kwa mikoa yote ya Zanzibar kutoka Januari hadi Machi mwaka huu, kati ya hizo 203 ni za  kubaka, 69 kulawiti na sita ni za kunajisi.

Kati ya kesi hizo kesi 224 zinaendelea na uchunguzi, 44 zipo

mahakamani na 10 zimefungwa kwa sababu mbali mbali.

Mwanaharakati, Zimamu Yussuf Salum wa Jambiani, Mkoa wa Kusini

Unguja, amesema wamekuwa wakipata shida wanapofika vituo vya Polisi

kuripoti kesi.

Aliyataja miongoni mwa matatizo wanayokutana nayo ni kuambiwa hakuna usafiri, hali inayopelekea wao au walalamikaji kutumia usafiri wa kukodi.

Alisema kuwepo kwa hali hio inawapa shida wasiokuwa na uwezo wa kulipia usafiri na matokeo yake safari yao ya kutafuta haki huishia njiani.

Zamimu alielezea kufurahishwa na kuona jamii inafunguka na kuwa na mwamko

mkubwa wa kuripoti makosa hayo, tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma.

 SERIKALI

 Katka hotuba yake ya  makadirio ya mapato na matumizi ya Afisi ya

Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la wawakilishi

Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2021/2022, Makamo wa Pili wa Rais, Hemed

Suleiman Abdulla, alisema licha ya jitihada zinazochukuliwa na

Serikali katika kupambana na ukatili wa kijinsia na udhalilishaji kwa

makundi mbalimbali ya kijamii, bado vitendo hivi vinaendelea.

Alifahamisha kwa mujibu wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali

na Jeshi la Polisi hapa Zanzibar, kwa mwaka 2020 kumeripotiwa matukio

1,363 (wanawake 217 na watoto 1,146) yanayohusiana na vitendo vya

ukatili na udhalilishaji.

Alisema katika kipindi cha miezi mitatu (Januari – Machi 2021) matukio

362 (wanawake 48 na watoto 315) yaliripotiwa, idadi ambayo ni kubwa

mno.

Kwa hivyo, alisema Serikali bado ina kazi kubwa ya kufanya katika kudhibiti

vitendo hivyo viovu.

“Wanaofanya vitendo hivi wamo katika jamii, lakini wanawaficha au tunayaficha kwa sababu ya muhali uliokuwepo”, alisema.

Takwimu zinaonesha Wilaya ya Mjini inaongoza kwa kiasi kikubwa kuwa na

matukio hayo ikifuatiwa na Wilaya za Magharibi ‘A na B’ na kwa hivyo ipo

haja ya kuweka nguvu zaidi za kupambana na vitendo hivyo sambamba na

kuchukua hatua kwa watakaobainika kufanya vitendo hivyo.

Alitahadharisha jamii kuelewa kwamba kitendo cha kumficha muhalifu

kina maana unashirikiana nae katika uhalifu huo na kuitaka

kuondoa muhali na kuripoti vitendo hivo.

Viongozi katika Shehia, Wilaya na Mkoa wakumbuke moja ya majukumu yao

ni kupunguza au kuondosha kabisa vitendo vya udhalilishaji kwa

wanawake na watoto katika maeneo yao.

“Tutaendelea kutengeneza mikakati ya kimawasiliano ili kuleta

mabadiliko ya tabia na kuihamasisha jamii kuongeza kasi ya kupambana

na vitendo hivyo kwa kutumia mikutano, mihadhara na vyombo vya habari,

kuyawezesha mabaraza ya watoto ya Shehia na Vilabu vya skuli

kujitambua na kuripoti matukio kama haya”, alisisitiza.

Jambo muhimu hivi sasa ni kuwepo kwa mashirikiano kati ya jamii na

taasisi mbali mbali katika kuhakikisha matendo hayo yanapunguwa au

kuondoka kabisa.

Kwa kushirikiana na Serikali na taasisi zake wana jamii watakuwa

wanatengeneza mazingira mazuri ya maisha kwa akina mama na watoto

ambao hivi sasa wanakabiliwa na hili janga la udhalilishaji.

Kwa upande mwengine jamii inapaswa kuwa makini, kuwaangalia watoto wao

na kufuatilia nyendo zao ili kuwakinga na janga hili la udhailishaji.