NA KHALEED SAID SULEIMAN, TORONTO CANADA
KUNA mtazamo unaoeleza kuwa Zakatul Fitr ni sadaka ya utakaso wa kufungua saumu ambapo huwa ni kiwango fulani cha chakula kinachotolewa na Waislam kwa Waislam katika siku chache za mwisho wa Ramadhan au siku ya Idi asubuhi, kabla ya kusaliwa Sala ya Idi.
Aidha, watetezi wa mtazamo huu wanaeleza kuwa Mtume Muhammad (SAW) na Maswahaba zake wakitoa Zakatul Fitr kwa vitu kama Ngano, Tende, Maziwa ya mgando au Zabibu kavu na kwamba hawajuzishi utoaji wa Zakatul Fitri kwa njia ya pesa na kushurutisha kuwa Mchele ndio umekubaliwa kuwa sadaka inayojuzu kutolewa kwa kuwa ndio chakula kikuu cha Mji au Nchi.
Pamoja na kuwepo kwa mtazamo huo ambao bila ya shaka yoyote na uheshimu na nawaheshimu watetezi wake kwa vile wamepitisha jitihada kubwa kutafiti mas-ala haya.
Katika kuelezea hali hiyo mambo haya yafuatayo yanahusu hili.
Falsafa ya sheria ya Kiislam (Usuul al Fiqh) ina kanuni mbali mbali. Moja wapo ni ile isemayo: mambo ni kwa makusudio yake (al umuuru bimaqaa swidihaa).
Kama hivyo ndivyo, hivi makusudio ya kumpa Mchele maskini wa Kiislam kwa ajili ya siku ya Idi ni yepi? Bila ya shaka yo yote ni kuwa na yeye afurahike siku ile kama wanavyofurahika wengine.
Je, kumpa Mchele peke yake kutamfurahisha kweli (hata apate gunia zima)? Na kwani Mchele ni chakula au ni nafaka? Na je, mtu mmoja si anaweza kupewa Zakaatul Fitr na mtu zaidi ya mmoja?
Sasa itakuwa ni Michele tu inayorundikana? Mchele ambao hauna makaa, hauna nazi, hauna kitoweo na kadhalika utapikwa vipi ugeuke chakula? Kwani Mchele unalika kama ulivyo au unahitajia kupitishwa katika hatua tofauti ili kugeuka chakula ndio uweze kulika?.
Na kwa kuwa wanaopewa Zakatul Fitr ni watu ambao hawana uwezo ndio ikaamuliwa nao wapewe, hivyo vitu vyengine vya kuufanya Mchele ugeuke chakula (Biriyani au Pilau mathalan) watavitolea wapi ikiwa kila mtoaji Zakatul Fitr atatoa Mchele?