KWA hali ya kawaida kila klabu inapopambana kuhakikisha inaingiza timu yake kwenye Ligi Kuu inakuwa na malengo.
Zipo timu kwenye ligi hazina chengine zinachofikiria zaidi ya ubingwa, lakini, pia zipo zinazotafuta tu nafasi ya kucheza michuano ya kimataifa ambayo nafasi ni mbili.
Kwa mpira wa miguu, si klabu tu bali hata timu za taifa unapotafuta kocha ni lazima ujue malengo ni nini, vyenginevyo ni wazi hakitatokea kile ambacho uongozi unakitarajia kuhusu matokeo ya uwanjani.
Sote tunatambua mpira wa miguu ni biashara kubwa na nzuri, hivyo kwetu sisi tunaona bado kuna kila sababu kwa klabu zetu kuwa na malengo ya kuwekeza zaidi kwa timu za vijana.
Lakini vile vile kuwekeza huko kwenye vijana ni biashara nzuri ingawa inahitaji kusubiri na uvumilivu wa kutosha ili kutoa mchezaji au wachezaji wanaoweza kupeleka faida katika klabu husika na pia timu ya taifa.
Kuajiri makocha kwa ajili ya ubingwa tu hakuna faida kinyume na kuwaajiri kwa ajili ya programu za vijana. Programu za vijana ni uwekezaji mzuri ingawa matunda yake yanachukua muda mrefu kuonekana, lakini, yakishaonekana yatadumu kwa muda mrefu na taifa kujivumia kwa hatma ya baadaye.
Mpira wa miguu kama ilivyo michezo mengine nguzo yake kubwa ni kuwa na wachezaji ambao uwezo wao wa kucheza na kasi viwe ni vitu vinavyoongezeka badala ya kupungua.
Kwa mantiki hiyo, wanahitajika zaidi wachezaji vijana, kwa vile hao ndiyo miili yao inaruhusu wawe na kasi uwanjani kuliko wachezaji waliokwishapita umri.
Lakini hilo litategemea vipi klabu imejipanga,ikiwa kwa malengo mafupi inaweza kuwa na wachezaji wa umri mkubwa ikijivunia uzoefu wao kwenye mchezo huo.
Lakini ikiwa kwa malengo ya siku za mbele, nafasi za wakongwe zinakuwa chache na hilo ndilo linaloonekana kwa klabu zetu nyingi.
Uzoefu unatuonesha kuwa hapa nchi kwetu, klabu zetu nyingi hazina timu za vijana hali ambayo inapelekea kila mwaka kusajili wachezaji wapya tofauti na mataifa yalioyoendelea kimichezo.
Ingawa klabu hizo nazo wakati mwengine hulazimika kusajili kwa gharama kubwa, lakini, hilo la kuwa na timu za vijana ni la msingi na lenye kufanyiwa kazi kikweli kweli.
Utayari wa klabu kuwekeza kwa vijana na pengine kukosekana kwa wachezaji vijana wenye msingi mzuri wa soka ili waweze kuwatumia katika timu zao ni kikwazo katika maendeleo ya baadaye ya klabu na taifa kwa ujumla.
Sasa lazima tufikie mahali na kuweka mikakati ya kweli katika kuzishajiisha klabu kuwa na timu za vijana ikiwa kweli tunahitaji mustakabali mwema wa soka hapa nchini kwetu.
Inawezekana tutimize wajibu wetu.