SIKU chache zilizopita rais wa Uganda, Yoweri Museveni aliapishwa kuendelea kuiongoza Uganda, kwenye hafla ambayo wakuu wa nchi 10 walihudhuria.
Museveni ataiongoza Uganda kwa miaka mengine mitano, ikiwa ni muhula wake wa sita mtawalia madarakani, ikikumbukwa kuwa aliingia madarakani mnamo mwezi Januari mwaka 1986 kwa mapinduzi ya kijeshi.
Katika awamu yake mpya aliyoianza itahitimika mnamo mwaka 2026 ambapo nchi hiyo itaandaa uchaguzi mwengine wakati ambao Museveni atakuwa tayari ameshakaa madarakani kwa miaka 40.
Museveni yupo katika kundi moja na rais wa Guinea ya Ikweta Teodoro Obiang, rais wa Cameroon Paul Biya, rais wa Jamhuri ya Congo (Brazzaville) Denis Sassou Nguesso na rais wa Eritrea Isaias Afwerki.
Ni orodha ya marais wakongwe barani Afrika ambao hadi sasa bado wapo madarakani. Kwa Afrika Mashariki Museveni anashika bendera kwa kuwa mtawala wa muda mrefu.
Alishinda uchaguzi wa Januari 14 mwaka huu kwa kuwabwaga wagombea wengine 10 waliowania nafasi ya urais kwa ushindi wa asilimia 58 ya kura zote.
Mbio za Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine za kumtoa madarakani Museveni ziligongwa mwamba, japo wapinzani, waangalizi wa kimataifa na makundi ya haki za binaadamu kudai kuwa uchaguzi huo uliingiliwa na serikali ya Museveni na kuminya wagombea wa upinzani.
Chini ya chama chake cha National Resistance Movement (NRM), Museveni ana nguvu za kisiasa, chama hicho kimeshinda wingi wa viti vya ubunge katika bunge la tisa, licha ya kushindwa katika baadhi ya ngome zake na chama cha NUP.
Uganda haijawahi kushuhudia ubadilishaji wa madaraka kwa njia ya amani tangu wakati wa marais waliopita Edward Mutesa, Milton Obote, Idd Ami, Yusuf Lule, Godfrey Binaisa, Paulo Muwanga, Bazilio Olara Okello, Generali Tito Okello na Museveni.
Viongozi wanaoingia madarakani nchini humo wanaingia madarakani kwa kutumia mfumo wa mwenye nguvu mpishe, taifa hilo limepita katika tawala za kijeshi na kiraia, mapinduzi, vita na machafuko. Baadhi ya watawala hao majina yao siyo maarufu kwa sababu hata mwaka haukutimia vyema waliondoshwa madarakani.
Hadithi ya Museveni ni tofauti kidogo kwani amewashinda watangulizi wake na kudumu muda mrefu na kuiweka nchi katika amani na kuinusuru na migogoro ya kisiasa na kikabila. Hujitapa kwa mafanikio hayo, kwa kusema Uganda haiendeshi tena siasa kwa sera za dini na makabila.
Bahati mbaya, mafanikio hayo yamekuja na gharama yake ambayo ni kukandamiza demokrasia na kutumia vibaya vyombo vya usalama. Ukandamizaji huo ni kama chakula kinachomfanya azidi kunenepa na kuongeza nguvu.
Nguvu zake haziishii hapo kwani chama chake cha NRM kina ushawishi mkubwa katika vyombo vya usalama, ushawishi huo ndio unaomuhakikishia kuendelea kuwa hai madarakani bila misukosuko kama watangulizi wake.
Mnamo Disemba 2020, mwezi mmoja kabla ya uchaguzi mkuu, Museveni alimteua mwanawe wa kiume, Luteni Jenerali Muhoozi Kaine-rugaba kuwa kamanda wa kikosi maalum cha ulinzi wa rais.
Muhoozi ana uzoefu mkubwa na shughuli za kiusalama, amewahi kuhudumu nchini Somalia katika kikosi cha Umoja wa Afrika, AMISOM kulinda amani, uteuzi wake zilikuwa hesabu za Museveni kujihakikishia usalama wakati taifa likiingia katika uchaguzi.
Nguvu zake kisiasa zitaendelea kuwepo ndani ya miaka mengine mitano ya uongozi wake, ingawa baada ya kutimiza miaka 81 mnamo mwaka 2026 kutakuwa na kitendawili ikiwa ataingia katika uchaguzi tena au atapumzika ama atapumzishwa.
Nguvu alizonazo atazitumia kuendelea kuituliza nchi. Kwa upande mwingine atazitumia kupambana na wapinzani wake kisiasa. Kwa hakika anajua vyema kucheza karata ya kuendelea kubaki madarakani bila kitisho chochote.
Demokrasia na Uchumi, “Hatutonyamazishwa, Museveni anapaswa kuondoka.” Ndivyo linavyosomeka moja ya makumi ya mabango kutoka kwa wafuasi wa Bobi Wine walioandama nchini Uingereza, Ijumaa ya tarehe Mei 8, 2021.