NA MARYAM HASSAN

JUMLA ya taasisi 29 za serikali na binafsi zimefanyiwa ukaguzi na Kikosi cha Zimamoto na Uokozi kuanzia mwezi Febuari mwaka huu hadi Aprili.

Kati ya taasisi hizo serikalini zipo 16 na 13 binafsi ambapo kikosi hicho kimebaini kasoro mbali mbali zimebainika ikiwemo uchakavu wa vifaa vya kuzimia moto (Fire Extingusher).

Taarifa hizo, zimetolewa na Mrakibu Msaidizi wa kikosi hicho Mohammed Juma Muhidini wakati akizungumza na Zanzibar Leo huko Ofisini kwake Kilimani ambapo katika taasisi hizo zipo baadhi yake vifaa vya kuzimia moto vimepitwa na wakati, ambapo walitakiwa kurekebisha haraka kasoro hizo.

Alisema katika ukaguzi huo zipo baadhi ya taasisi zimeshindwa kutoa ushirikiano, jambo ambalo limepekelea kushindwa kufikia lengo.

“Hii haipendezi kwa baadhi ya taasisi kushindwa kutupa ushirikiano kwa sababu sisi kikosi kawaida tunaweka mipango yetu ikiwa tumepanga kukagua taasisi sita kwa siku tunashindwa na badala yake tunapata taasisi mbili tu huku tukipoteza muda kuwasujudia watendaji hao” alisema.

Aidha alisema katika ukaguzi huo pia wamekagua maduka ya gesi 102 yaliyopo barabarani, na mitaani ambapo changamoto kubwa waliyoibani ni kuwa baadhi yao hawana vyeti ambavyo vimetolewa na Zimamoto.

Alisema kawaida kikosi hicho hutoa mafunzo kwa wauzaji na wasambaji wa gesi, na pia huwapa vyeti maalum ambavyo vinaweza kupatiwa leseni ya biashara.

Sambamba na hayo, alisema changamoto nyengine ni uwekaji mbaya wa mitungi ya gesi na bidhaa za vyakula jambo ambalo ni hatari kwa jamii.

“ Hapa utaona ndani ya duka imo mitungi ya gesi, pembeni zipo katuni za maji au juisi na mda mwengine utakuta kibiriti cha kuwashia sigara kimetundikwa hii ni hatari mana hapa moto ukitokea hakuna wa kumlaumu” alisema.

Inspekta Haji Khatib Hassan, alisema ni vyema taasisi na sekta binafsi kuhakikisha wanatoa ushirikiano pindi wakaguzi wa kikosi hicho wanapofika katika maeneo yao kwa ajili ya ukaguzi.

Aidha alisema kabla ya kuanza matumizi ya gesi lazima kufuata sheria, ili kupunguza matukio ya moto ambayo yapo baadhi yao yanatokana na gesi.