Asema ZSTC imesahau wajibu wake

NA HAJI NASSOR, PEMBA

MAKAMU wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud Othman, amebainisha mambo kadhaa yanayochangia kupungua uzalishaji wa zao la karafuu, ikiwemo utaalamu hafifu wa uoteshaji miche na Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar (ZSTC) kushindwa kutekeleza wajibu wao kwa wakulima.

Alisema, huwa kunatangazwa idadi kubwa ya uzalishaji na ugawaji wa miche ya zao hilo kwa wakulima, hata hivyo hakuna takwimu sahihi za miche mingapi inayooteshwa na wakulima inaota, huku pia wakulima wengi kupanda kwa mazoea.

Makamu huyo wa Kwanza, aliyasema hayo Kiwanda cha Makonyo Wawi Chake chake, alipokuwa akizungumza na wakulima na wadau wa zao la karafuu, ikiwa ni sehemu ya ziara yake kisiwani Pemba.

Alisema, jengine linalosababisha mikarafuu kupotea ni wale waliokabidhiwa mashamba ya eka tatu, kutoyashugulikia ipasavyo, jambo ambalo mengine ilipoteza uhai kabla ya wakati wake.

Kuhusu ZSTC, alisema imekuwa ikikurupuka na kujiweka tayari wakati wa uvunaji wa zao hilo pekee, na kuwaacha wakulima katika muda wote wakihangaika wenyewe.

“ZSTC imekuwa kama vile sheikhe anaemuoezesha mume mtoto wa nje ya ndoa, ambapo baada ya ndoa hampitii tena kumpa elimu, anachosubiri ni kuvunjika kwa ndoa hiyo na kumfungisha ndoa nyingine,’’alisema kwa kutolea mfano.

Alisema, zao la karafuu halihusu uvunaji na bei pekee, bali kwa mfano ZSTC, ilipaswa kuwa karibu na wakulima wakati wote, ili kufuatilia mwenendo wa uoteshaji, usafishaji mashamba hadi kufikia siku ya kuvuna.

“Hata ukiona ZSTC wanashughulikia vituo vya mauzo, kununua kamba, majamvi ujue hapo mavuno ya karafuu tayari, lakini wakati mkulima anataka kushughulikia shamba lake hawaonekani”, alifafanua.

Aidha alilalamikia tabia ya baadhi ya wakulima, waliorithi ama kukabidhiwa mashamba ya eka tatu kutoyashughulikia na kusababisha kushuka idadi ya tani za karafuu kwenye soko la dunia.

“Kila mmoja ni shahidi kuwa, mnamo mwaka 1830, Zanzibar iliuza tani 35,000 soko la dunia, lakini kutoka hapo ikawa kila mwaka inashuka hadi miaka 1970 kuzalisha tani kati ya 15,000 hadi 16,000, alifafanua.

Hata hivyo Makamu huyo wa Kwanza wa Rais, alisema sasa serikali ya awamu ya nane, inayoongozwa na Dk. Mwinyi imejipanga kulifufua na kuliendeleza zao hilo kwa vitendo.

Katika hatua nyingine, Makamu huyo wa Kwanza, amewaagiza wakuu wa wilaya na mikoa kisiwani Pemba, kuendelea kuimarisha ulinzi wa zao hilo, ambalo haitawasumbua wakulima.

“Imekuwa ni tatizo wakati wa uvunaji wa zao la karafuu Pemba, hata mkulima hana furaha, maana akiliacha shambani linaibiwa, akilichuma anapata changamoto kulipeleka eneo jengine,’’alieleza.

Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya wazalishaji Karafuu Zanzibar ‘ZAPCO’ Abubakar Mohamed Ali, alisema wakulima wamejisikia unyonge wanapoyaendeleza mashamba ya eka tatu, kisha kuchukuliwa na serikali.

Alisema, wapo wakulima waliokabidhiwa eka tatu tatu, na kuyaendeleza mashamba na wengine hadi kupanda mikarafuu 300, wamepokonywa kwa njia ya kulazimishwa kuyakodi nje ya uwezo wao.

Alimueleza Makamu huyo wa Kwanza kuwa, lazima serikali iwe makini inapoyatafuta mashamba ya eka tatu na sio kuchukua mashamba yaliyomea na kuyafanya ni ya serikali bila ya kumjali aliyefyeka pori.

Naye Mkulima Muhene Ali Salim, alisema wakulima walio wengi wanaiotesha mikarafuu baada ya kukabidhiwa na serikali kinyume na maagizo ya wataalamu wa kilimo hicho.