NA KHAMISUU ABDALLAH

WATU 26 wamekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi wakiwa wanasafirisha mazao bila ya kuwa na kibali.

Akizungumza na vyombo vya habari kituo cha Polisi Mwera, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Awadh Juma Haji, alisema watu walikamatwa baada ya jeshi hilo kufanya operesheni za mara kwa mara katika mkoa wake.

Alisema ikiwa jeshi lake lipo katika kufanya operesheni za kukabiliana na uhalifu ikiwemo uhalifu wa matukio ya wizi wa mazao ya kilimo wanavunja sheria za nchi ikiwemo kukwepa kulipa kodi.

Aidha alisema hivi karibuni kumeibuka matukio ya wizi wa mazao unaofanywa na baadhi ya watu kutoka maeneo mbalimbali kuiba mazao na kuyapeleka katika masoko kwa ajili ya kujipatia kipato kwa njia zisizokuwa halali.

Alisema kufuatia hali hiyo Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi limeanza operesheni hiyo ili kukabiliana na vitendo vyote vya uhalifu ikiwemo uhalifu huo.

Kamanda Awadh, alisema watu hao wakiwa katika gari tano tofauti aina ya ‘Carry’ walipatikana wakiwa wamepakia mazao hayo ambayo hayana kibali wakielekea sokoni kwa ajili ya kuuza.

Alisema kwa mujibu wa sheria za Zanzibar mtu yoyote anaetaka kusafirisha mazao kutoka sehemu moja kwenda nyengine ni lazima awe na kibali kutoka kwenye mamlaka zinazohusika kuonesha uhalali wa mazao hayo.

Alisisitiza kuwa kila mmoja atawajibika kuonesha uhalali wa mazao hayo na atakaeshindwa atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.

ACP Awadh alibainisha kuwa baada ya mahojiano na baadhi ya watu wamedai kuwa walikwenda kwa masheha wa sehia zao na kudai kuwa hawana vibali.

Mbali na hayo, Kamanda Awadh, aliwataka masheha na viongozi wengine wenye dhamana ya kutoa vibali kutimiza wajibu wao wa kuwapa vibali wananchi ili kuwaondolea usumbufu.

Alitoa onyo kwa madereva wanaosafirisha mazao kuhakikisha wanabeba mizigo kulingana na uwezo wa gari zao na yoyote atakaekamatwa akiwa amezidisha mzigo basi atachukuliwa hatua.

Kamanda Awadh alibainisha kuwa operesheni hiyo itakuwa endelevu kwa barabara zote zinaozoingia na kutoka katika mkoa wa Mjini Magharibi na kuwataka watu wanaotoka mikoa jirani kuhakikisha wanafuata taratibu na sheria zilizokuwepo.

Katika hatua nyengine Kamanda Awadh, alisema mbali na operesheni hiyo pia jeshi lake linaendelea na operesheni nyengine ya nyumba kwa nyumba kwa watu wanaojihusisha na matukio ya uporaji, uvunjaji wa nyumba hasa kwa maeneo ambayo yameanza kukithiri kwa vitendo vya kihalifu.

Aidha alitoa onyo kwa wahalifu kuacha mara moja vitendo hivyo na badala yake kujishughulisha na shughuli zilizokuwa halali na kuwaomba wazazi wenye vijana wenye umri wa miaka 20 hadi 25 kuwatafutia kazi halali vijana wao.

Nao baadhi ya watu waliokamatwa na mzigo huo walisema walikwenda kwa sheha kwa ajili ya kupata kibali lakini waliambiwa hakuna.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima wenziwe Mcha Ali Manzi, ambae ni mkulima wa ndimu katika kijiji cha Chwaka, aliipongeza serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi ambayo inatekeleza wajibu wake kwa kutumia sheria, katiba na sera.

Alisema tukio lilijitokeza kwao hawalioni kwamba ni kikwazo kwani Jeshi la Polisi limetumia haki ya kikatiba na sheria za nchi kulisimamia zoezi hilo linaloendeshwa kinyume na utaratibu kwa kupoteza mapato kwa ajili ya uchumi wa wananchi wa Zanzibar unaotokana na baadhi ya watendaji kutowajibika katika majukumu yao.

Alitoa wito kwa ngazi za Sheha, Wilaya na Mkoa kuwajibika kama linavyowajibika Jeshi la Polisi katika kusimamia haki zote za kisheria ambazo zinaleta kikwazo kwa wananchi wa chini ambao hawajui utaratibu wa sheria na katiba.

Waliliomba Jeshi la Polisi kushuka katika ngazi hizo kwa ajili ya kushajihisha jambo hilo kwani wananchi wapo tayari kufuata sheria na katiba hasa suala la kulipa kodi.

Walisisitiza kuwa ni vyema kwa serikali kulichukulia uzito suala hilo ili kuona kila mwananchi anafanya shughuli zake za kujipatia kipato bila ya usumbufu wowote