NA PRISCA LIBAGA, ARUSHA
MKUU wa Mkoa wa Arusha, Iddi Kimanta amezindua miradi katika sekta ya kilimo na elimu yenye thamani ya zaidi ya milioni 820 iliyofadhiliwa na kutekelezwa na shirika la World Vision katika halmashauri ya wilaya ya Meru, wilayani Arumeru.
Alphonce Kirarija kutoka shirika hilo ameitaja mradi hiyo kuwa ni kilimo cha umwagiliaji katika Kijiji cha Shambarai ambao umegharimu shilingi milioni 422 na miradi yenye thamani ya shilingi milioni 406 katika skuli za msingi Kerikenyi ya ujenzi wa nyumba ya walimu (two in one), ujenzi wa vyoo vya wanafunzi vyenye matundu 20, tanki la kuhifadhia maji na karo la kunawia mikono.
Aidha, Kimanta alipongeza shirika hilo na kuwataka wananchi kulinda na kuisimamia miradi hiyo “hakuna haki bila wajibu”, amehimiza.
Pia, Kimanta aliahidi kuchangia ujenzi wa ofisi ya walimu katika skuli ya msingi Kerikenyi kwa kutoa matofali 1,500 na mkuu wa wilaya kutoa saruji. Aidha, Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru umeahidi kuchangia vifaa katika hatua za ukamilishaji.
Mkuu wa Mkoa alihitimisha kwa kuwaagiza wenyeviti wa vijiji kuhakikisha wanasoma taarifa za mapato na matumizi ili kuongeza ari ya wananchi katika kuchangia miradi ya maendeleo.
Mkuu wa wilaya ya Arumeru Jerry Muro ameahidi kuendelea kushirikiana na wadau pamoja na Wananchi kuhakikisha miradi hiyo inakuwa na tija.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya amepongeza utendaji wa Serikali katika jitihada za kuinua Wakulima kiuchumi.
Aidha, katika ziara hiyo Kimanta aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mkurugenzi wa World Vision Tanzania, Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Meru Emmanuel Mkongo.