JUBA, SUDAN KUSINI

RAIS wa Sudan Kusini, Salva Kiir ameshindwa kutimiza usawa wa kijinsia katika serikali mpya ya umoja wa kitaifa aliyoiunda hivi karibuni pamoja na kwenye bunge la nchi hiyo.

Taarifa kutoka nchini humo zinaeleza kuwa kati ya wabunge 550, rais huyo ameteua wabunge 116 wanawake suala ambalo linalalamikiwa kuwa hakutilia maanani suala la kuwainua wanawake.

Hatua ya rais Kiir kushindwa kuwapa nafasi wanawake, imelalamikiwa na taasisi za utetezi wa haki za wanawake nchini humo baadhi yao wanetoa maoni yao kwenye mitando ya kijamii kuonesha kutoridhishwa na hali hiyo.

Mwezi Februari mwaka jana katika ya mawaziri 35 aliowateua kuunda serikali wanawake walikuwa 10, ambapo katika serikali mpya ya umoja wa kitaifa aliyoiunda wanawake ni wachache.

Katika uteuzi wa magavana 10 alioufanya mwezi Julai mwaka jana aliteua gavana mmoja mwanamke ambaye pia alipendekezwa na makamu wa rais wa nchi hiyo Riek Machar.

Edmund Yakani, ambaye ni mkuu wa jumuiya ya uwezeshwahi wa jamii nchini humo, alisema kuwa rais huyo amewasahau wanawake kuwapa nafasi za uongozi na ni jambo la kusikitisha sana.