NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amepangua wakuu wa mikoa na kuteua watendaji katika taasisi mbali mbali za serikali.

Taarifa yake iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Gerson Msigwa, imesema uteuzi huo umeanza jana na viongozi hao wataapishwa Mei 18 mwaka huu ikulu jijini Dar es Salaam.

Katika uteuzi huo, baadhi ya viongozi wameondolewa katika mikoa waliyokuwa wakiiongoza na baadhi yao kufikia umri wa kustaafu.

Walioteuliwa ni Anthony John Mtaka kuwa mkuu wa mkoa wa Dodoma kabla ya uteuzi huo alikuwa Simiyu na Zainab Rajab Tekcla kuwa mkuu wa Mkoa wa Lindi awali alikuwa Shinyanga.

Wengine ni Mhandisi Robert Luhumbi, kuwa mkuu wa Mkoa Mara ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Geita, Juma Zubeir Homera, anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.

Rais Samia, pia amemteuwa Martin Reuben Shigella kuwa Mkuu wa Mkoa Morogoro, ambapo kabla ya Uteuzi huo alikuwa Mkuu wa Mkoa Tanga.

Wengine aliowateuwa ni Meja Jenerali, Marco Elisha Gaguti, ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, ambapo kabla ya uteuzi huo, alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera na anachukua nafasi ya Gelasius Gasper Byakanwa, ambaye atapangiwa kazi nyengine.

Samia, amemteuwa, Albert Charamila kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambapo kabla alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na Aboubakar Mussa Kunenge kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, ambapo hapo awali alikuwa Mkoa wa Dar es Salaam.

Samia amemteuwa Joseph Joseph Mkirikiti, kuwa  Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Manyara akichukua nafasi ya Joachim Leonard Wangambo ambaye amestaafu.

Wengine Dk. Binilith Satano Mahenge kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

Samia, amemteuwa Dk. Philemon Rugumiliza Sengati kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora na John Vanney Mongella kuwa Mkuu wa Mkoa Simiyu.

Pia amemteuwa Ally Salim Hapi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, ambapo kabla ya uteuzi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Adam Kigoma Malima anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga.

Arusha ameteuliwa David Zakaria Kafulila, ambapo anachukua nafasi Iddi Hassan Kimanta  ambaye amestaafu na Amos Gabriel Makalla anakuwa mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Rosemary Staki Senyamule ameteuliwa kuwa mkuu wa mkoa Geita, ikiwa anachukua nafasi ya Robert Gabriel Luhumbi ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Queen Cuthbert Sendiga anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Amemteuwa Brigedia Jenerali Charles Mbuge kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, anachukua nafasi ya Meja Jenerali Marco Elisha Gatuti na Mwanamvua Mrindoko kuwa Mkuu wa Mkoa Katavi.

Samia, pia amemteuwa Stephen Kagaigai kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ambapo hapo awali alikuwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Brigedia  Jenerali, Wilbert Augustine Ibuge ameteuliwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ambaye anachukua nafasi ya Christine Mndeme ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM.

Wengine ambao Rais Samia amewateuwa ni Omary Twebweta Mgumba kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe na Makongoro Nyerere kuwa Mkoa wa Manyara.

Wengine amemteuwa Thobias Emir Andengenye kuwa Mkuu wa Kigoma, ambaye anaendelea na wadhifa wake kwa Mkoa huo, na Marwa Mwita Rubirya, anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe.

Upande wa uteuzi katika taasisi, Samia, amemteuwa Balozi Joseph Edward Sokoine kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Samia amemteuwa Nenelwa Mwihamba kuwa Katibu Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwa anachukua nafasi ya Stephen Kagaigai ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Dk. Edwin Paul Mhede ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Kasi (UDART) akiwa anachukua nafasi ya John Nguya  ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Amemteuwa, Sylevester Antony Mwakitalu kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka, (DPP) ambaye anachukua nafasi iliyoachwa na Biswalo Mganga ambaye ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu na Naibu wake atakuwa ni Joseph Pande akiwa anachukua nafasi ya Edson Athanas Makallo, ambaye atapangiwa majukukumu mengine.

Rais Samia amempandisha Cheo cha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Salum Rashid Hamdani kuwa (CP) na anakuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, (TAKUKURU).