Asema amebeba jukumu kubwa

NA KHAMISUU ABDALLAH

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewaomba watanzania kuendelea kumuombea ili aweze kumpa nguvu na uadilifu katika kutekeleza majukumu yake ya kuwatumikia watanzania.

Kauli hiyo aliitoa katika hotuba yake iliyosomwa na Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma, katika dua ya pamoja ya kumuombea Samia na taifa kwa ujumla iliyoandaliwa na wanawake wa kiislam Zanzibar katika ukumbi wa Michenzani Mall.

Samia, alisema anahitaji dua za wananchi kwani mzigo aliopewa ni mkubwa wa kulitumikia taifa la Tanzania. Aidha, alisema kila binadamu ana mapungufu yake, lakini dua za watanzania ndio zitakazomsaidia kutimiza matarajio yake kwa wananchi.

“Kuna mambo ambayo yanaweza yakatokezea, lakini jamii ikiendelea kumuombea dua basi Mungu atayapa tahfifu,” alisema.

Alisema hiyo ni shani kubwa waliopewa wanawake hivyo ni vyema kuendelea kumuunga mkono katika jukumu kubwa la kuwatumikia wananchi.

Sambamba na hayo, alimuomba Mwenyezi Mungu kumpa nguvu za kutekeleza majukumu yake kwa urahisi katika kuwapatia maendeleo wananchi ya haraka kama dhamira ya kiongozi wake aliyetangulia mbele ya haki Dk. John Pombe Magufuli na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi.

Akifungua dua hiyo Mwalim Thania Mahmoud, alisema shughuli hiyo ni muhimu kwa kiongozi wao mwanamke ambae amepata nafasi kubwa anaetoka Zanzibar kuliongoza taifa la Tanzania na anatakiwa kushukuriwa ni Mwenyezi Mungu pekee.

Alimuomba Mwenyezi Mungu ampe mafanikio na kuondoa mahasidi na maadui wabaya katika uongozi wake ili aweze kutekeleza majukumu yake katika kuinyanyua nchi katika mambo ya kimaendeleo.

Akitoa maelezo mafupi kwa niaba ya wanawake wa kiislam Zanzibar, Sabra Issa Machano, aliwaomba wanawake wenzake kumpa ushirikiano kiongozi huyo na kuacha tabia ya kuvunjana moyo na kudharauliana.

“Hatujawaza kama mwanamke anaweza kupata uongozi mkubwa, hii ni kudra ya Mwenyezi Mungu imeshukia na alipangalo Mungu binaadamu huwezi kulipangua”, alibainisha.

Alisema Samia sio kiongozi wa mwanzo mwanamke kwani wapo wanawake ambao walikuwa viongozi ikiwemo bi Khadija ambae alikuwa mke wa Mtume Muhammad (S. A. W), bi Asya, bi Maryam, bi Fatma na bi Aisha ambao walifanya kazi kubwa katika kuiendeleza dini ya kiislam.

“Uislam ulitoa nafasi kubwa hasa kwa viongozi wanawake ambao waliisimamia dini yetu na sisi tumejifunza kutoka kwao na yeye tunaamini Mwenyezi Mungu ampe nguvu na uwezo mkubwa kuifikisha nchi yetu ambayo sisi hatuwezi kuikadiria”, alibainisha.

Wanawake hao walimuomba Mwenyezi Mungu kuendelea kumpa kheir na salama katika kazi zake na kumpa uwezo kama wanawake ambao waliifanya dini ya kiislamu iweze kufika katika hatua kubwa.

Mbali na hayo wanawake hao waliahidi kumuunga mkono, kumsikiliza, kumtetea na kusimamia yale yote ambayo anaamrisha kwa wananchi wake.

Hata hivyo walisema wanamuamini na kumkubali Samia kwani ana uwezo mkubwa wa kuwaongoza watanzania kwa kusimamia misingi ya umoja, usawa na mshikamano mkubwa.

Akitoa salam kwa niaba ya familia ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambae ni dada wa kiongozi huyo Mgeni Suluhu Hassan, aliwapongeza wanawake wa kiislam Zanzibar kwa dua hiyo.

Dua hiyo ilihudhuriwa na mamia ya wanawake mbalimbali wa kiislam kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya za Unguja.