ZAINAB ATUPAE NA ALLY HASSAN
WIZARA ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imesema inatoa mafunzo ya mara kwa mara kwa vijana, ili kupata vipaji vitakavyo itangaza nchi yao kupitia sekta ya michezo kitaifa na kimataifa.
Kaimu Waziri wa Wizara hiyo Lela Mohammed Mussa aliyasema hayo Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani, wakati akijibu suala la nyongeza lililo ulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Jang’ombe Ali Abdulgulam .
Mwakilishi huyo alitaka kujua wizara ina mpango gani wa kutoa mafunzo ya michezo, ili kupata vijana bora watakao itangaza nchi yao hasa mchezo mpira wa miguu.
Alisema wizara inajitahidi kutoa mafunzo kwa vijana ili kufanya vyema katika mashindano mbali mbali ambayo wanashiriki ngazi za kitaifa na kimataifa.
Waziri Lela akijibu swali la msingi lililoulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Nungwi Abdalla Abass Wadi, aliyetaka kujua wizara ina mpango gani wa kuzitembelea klabu za michezo za wilaya.
Waziri huyo alisema kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Michezo ya Taifa namba tano ya mwaka 2010, wizara ina mfumo wa michezo katika ngazi za wilaya.
Alisema katika kila wilaya, kuna Baraza la Taifa la Michezo chini ya uongozi wa mkuu wa wilaya.
Alisema mabaraza ya wilaya yanawasiliana na ofisi kuu ya utawala na uendeshaji wa shughuli za michezo kupitia ofisi ya Mrajis wa Michezo na msaidizi wake, wanafanya ziara mbali mbali katika wilaya.
Alisema mwaka huu, ofisi ya Mrajisi imefanya ziara wilaya zote nne za Pemba kuwaalika wadau mbali mbali wa michezo.
Akitoa mfano Lela alisema katika wilaya ya Wete kuanzia mwaka 1985/2020 jumla ya klabu 199 zilisajiliwa, lakini baada ya kutembelea wilaya hizo ofisi ya Mrajisi ilibaini kuwa klabu 44 ndizo vinazocheza mpira wa miguu.
Hata hivyo alisema sera ya taifa ya michezo ya mwaka 2018, imeeleza majukumu kwa wadau mbali mbali, katika kusimamia maendeleo ya michezo ikiwa ni pamoja na ofisi za mkoa, wilaya na shehia.
Sambamba na hayo alisema hayo yote yana lengo la kuona michezo katika ngazi za wilaya inaendelezwa.